come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SIMBA KWAZIDI KUWAKA MOTO, KAMATI YA NDUMBARO YAMFYEKA KABISA WAMBURA, YAMGOMEA MALINZI

Dk Ndumbaro kulia akizungumza leo
KAMATI ya Uchaguzi ya Simba SC imesema kwamba, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halina mamlaka kikatiba kusimamisha uchaguzi wa klabu hiyo, na maana yake uchaguzi huo upo kama ulivyopangwa kufanyika Juni 29, mwaka huu.


Pamoja na hayo, Kamati hiyo imesema imemuondoa moja kwa moja mgombea Michael Richard Wambura kwenye kinyang’anyiro hicho kwa sababu amerudia kosa ambalo aliwahi kupewa onyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katka ukumbi wa Serengeti, ndani ya hoteli ya JB Belmonte, Dar es Salaam mchana wa leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba SC, Dk Damas Ndumbaro  amesema kwamba Wambura amerudia kufanya kampeni kabla ya wakati.

TAARIFA KAMILI YA NDUMBARO;

Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, ilifanya mkutano wake kawaida tarehe 15 Juni 2014 kujadili mambo mbalimbali ambayo yanayohusu uchaguzi mkuu wa Simba Sports Club ambao umepangwa kufanyika tarehe tarehe 29 Juni 2014. Kamati ya Uchaguzi ya Simba sports Club inapenda kuujulisha umma, hususan wapenzi wa Simba Sports Club mambo yafuatayo:
Wanchama wa Simba SC, Geoffrey Nyange 'Kaburu' kushoto na Daniel Kamna kulia walikuwepo

1. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, kwa mujibu wa Ibara ya 10(6) ya Kanuni za uchaguzi za TFF toleo la mwaka 2013, ndiyo chombo pekee chenye mamlaka ya kutangaza, kubadilisha, kusimamisha au kufuta tarehe ya Uchaguzi ya Simba Sports Club. Kwakuwa Kamati haijafanya hivyo, wala hakuna mdau yoyote aliyeleta hoja ya kusimamisha uchaguzi, tunawajulisha kuwa uchaguzi wa Simba Sports Club upo pale pale kama ambayo Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilivyopanga. Maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vema na Uchaguzi utafanyika tarehe 29 Juni 2014 kama ilivyopangwa hapo awali.
2. Kamati imesikia kupitia vyombo vya habari kuwa TFF imesimamisha uchaguzi wa Simba Sports Club mpaka hapo Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club itakapoteua Kamati ya Maadili. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club inapenda kusema yafuatayo:

i. Mamlaka ya kusimamisha uchaguzi ni kazi ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kwa mujibu wa ibara 10 (6) ya Kanuni za Uchaguzi, 2013
ii. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilipoanza mchakato wa uchaguzi ilitoa tamko kuwa: “kwasababu Simba Sports Club haina kanuni za Uchaguzi, Kamati ya Rufaa ya uchaguzi, wala Kamati za Maadili kwa mujibu wa ibara za 16 (e) na (f) ya Katiba ya Simba Mwaka 2014, vyombo husika vya TFF vitatumika”. Kulikuwa hakuna pingamizi toka kwa mtu yoyote juu ya kauli hiyo, ikiwemo TFF.
iii. Tarehe 26 Mei 2013, Rais wa TFF aliialika Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club katika chakula cha mchana. Katika mkutano huo, kauli ya aya (ii) hapo juu ilirejewa na Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilikabidhi rasmi mchakato mzima wa uchaguzi na kutoa ufafanuzi kuwa kamati husika za TFF zitahusika, jambo ambalo halikupingwa na TFF.
iv. TFF iliruhusu Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF kusikiliza Rufaa za uchaguzi za Simba, hivyo basi haiwezi kuzuia Kamati zake nyingine kusikiliza Masuala ya kimaadili. “Estopel” inawazuia TFF kufanya hivyo sasa.
v. Wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club, isipokuwa watatu tu, ni wagombea katika uchaguzi huu. Na hao watoto tayari wapo kwenye Kambi za Kampeni za uchaguzi hii ambazo zipo bayana kabisa. Kuiagiza Kamati ya Utendaji ya Simba iunde Kamati ya Maadili kusikiliza kesi za maadili dhidi yao wenyewe ni kukiuka msingi wa haki ya asili (natural justice). Ni dhahiri kuwa haki haiwezi kutendeka kwa wajumbe wa kamati ya utendaji ya Simba Sports Sports Club, ambao ni watuhumiwa katika masuala ya maadili, wachague majaji wa kuwahukumu. Hapo haki haitatendeka.
Ifahamike kuwa, baada ya Kamati ya Utendaji ya Simba Sports Club kuteua Kamati ya uchaguzi ya Simba Sports Club, Kamati hiyo haina mamlaka tena ya kujadili, kuingilia au kuteua chombo kingine kufanya shughuli zinazohusu uchaguzi ukizingatia kuwa wajumbe wake ni wagombea.

vi. Katika Uchaguzi Mkuu wa TFF wa Mwaka 2013, ambao ulimuingiza Jamal Malinzi Madarakani, FIFA walikuja, wakongea na pande zote na hatimaye, walisema kuwa; “tunapendekeza kuwa uchaguzi mkuu usimame ili kuunda kamati mbalimbali”. Mapendekezo hayo yalipokelewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Bw. Deo Lyato, na hatimaye ni Kamati ya Uchaguzi ya TFF ndio iliyotangaza kusimamisha Uchaguzi na sio Sepp Blatter.

vii. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ni Kamati huru ambayo haipaswi kuingiliwa na Chombo chochote kile. Ili kulinda uhuru huo, tunalazimika kukanusha matamshi ya TFF kuhusu kusitisha Uchaguzi Mkuu wa Simba Sports Club. 
3. Malalamiko ya Kimaadili Kupelekwa FIFA.

Kwa mujibu wa Ibara ya 11 (9) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, 2013, inatoa mamlaka kwa Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kupeleka masuala ya maadili katika kamati ya maadili ya TFF. Tarehe 9 Juni 2014, Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilipeleka Masuala ya Maadili katika Kamati ya Maadili ya TFF. Kwakuwa TFF imekataa kusikiliza masuala ya maadili ambayo yanakiuka Kanuni za maadili, Katiba za Simba, TFF na FIFA, Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, itapeleka Masuala ya Maadili FIFA ili haki itendeke.

4. Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilijadili kuhusu vitendo vya wagombea kupiga kampeni kabla ya muda wa kampeni ulioruhusiwa. Kwa mujibu wa Mchakato wa Uchaguzi ya Simba Sports Club, muda wa kampeni unaanza tarehe 24 -28 Juni 2014. Hapo awali kamati ilibaini kuwa wagombea wawili wa nafasi ya urais; Michael Richard Wambura na Evans Aveva walifanya vitendo vya kampeni siku ya kuchukua na kurejesha fomu za kugombea. Tarehe 25 Mei 2014, Kamati iliwapa ONYO KALI la maandishi wagombea hao na kuwataarifu kuwa hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao, ikiwemo kuondolewa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi. 

Baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club kumuondoa Bw. Michael Richard Wambura katika kinyang’anyiro cha uchaguzi Mkuu wa SImba Sports Club, Bw. Wambura aliitisha Mkutano na waandishi wa habari, aliitukana Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club, na kutoa matamshi ambayo ni Kampeni.
Baadaya ya Kamati ya Rufaa ya uchaguzi ya TFF kumrejesha Bw. Wambura katika Kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa Simba, Bw. Wambura aliitisha tena mkutano wa waandishi wa habari, aliisifu kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF, kwa mara kwanza aliisifu Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club na kutoa matamshi ambayo ni wazi kuwa ni kampeni. Baadhi ya Matamshi aliyoyatoa kupitia vyombo vya habari ni kama ifuatavyo:

i. “Simba Sports Club inahitaji zaidi wadhamini na sio wafadhili”
ii. “Wafadhili kazi yao in kutoa fedha mfuko wa kushoto na kuepeleka mfuko wa kulia”

iii. “Simba ilikuwa na viwanja vitatu lakini kimoja kimeuzwa na wajanja na vimebaki viwili tu”
Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ilitafakari matamshi hayo, na kubaini kuwa hiyo ni kampeni ya waziwazi wakati muda wa kampeni bado haujaanza.
Kamati ya Uchaguzi ya Simba Sports Club ililipa jambo ili uzito wa kipekee kwasababu Mkosaji amekuwa na tabia ya kurudia kosa hilo hata baada ya kupewe onyo la maandishi.

HIVYO BASI: Kwa mujibu wa mamlaka ya kikanuni, hususan Ibara za: 6 (1) (a) – (g); 6 (1) (L) na 14(3) za Kanuni za uchaguzi za TFF – 2013, Bw. Michael Richard Wambura anaondolewa Katika Kinyang’anyiro cha Uchaguzi wa Simba Sports Club, 2013, kwa kosa la kurudia kufanya kampeni kabla ya muda wa kampeni ambao umepengwa,".