come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: MACHOZI YATANITOKA AKIONDOKA MADARAKANI KIKWETE

Na Fikiri Salum

JK akiwa katikati na wachezaji mahiri Mbwana Samatta kulia na Thomas Ulimwengu kushoto alipowatembelea hotelini Lubumbashi.
 MACHOZI yalinitoka siku rais wa awamu ya tatu mhe Benjamin William Mkapa alipokuwa anapungia mikono kuashiria anaaga Watanzania mwaka 2005 pale uwanja wa Uhuru 'Shamba la bibi'


Ilinibidi nitumie kitambaa kidogo 'Leso' kujifuta machozi yaliyoanza kunitoka kwa wakati huo hasa baada ya Mkapa kuuaga urais, Mkapa alifikia tamati baada kumaliza miaka yake 10 madarakani.

Unajua sababu gani iliyonifanya nitokwe na machozi? Mkapa aliasisi ujenzi wa uwanja wa soka wa kisasa ambao ni uwanja wa Taifa uliokamilika na kuzinduliwa mwaka 2006 na awamu ya nne inayoongozwa na Jakaya Kikwete.

Ndugu wasomaji leo mtanisamehe kidogo kutokana na mwanzo wa makala hii niliyoiandika, machozi yatanitoka akiondoka madarakani JK hasa baada ya kujionea mwenyewe kwa macho yangu rais huyo anavyokuwa bega kwa bega na wananchi wake bila ubaguzi wowote.

Sina zawadi ya kumtunuku zaidi ya kumsifu kupitia makala hii, Kikwete amekuwa rais wa kwanza kusaidia na kushirikiana na wapiga kura wake na vilevile amekuwa mstari wa mbele pale anaposikia msanii au mwanamichezo amepatwa na masahibu.

Hata anapokuwa nje ya nchi, JK anatuma salamu za kumjulia hali mgonjwa ama wafiwa, ameonyesha ukarimu huo kwa wanamuziki nguli Muhidini Gurumo na DK Remmy Ongala ambao wote ni marehemu.

Kikwete alienda kuwajulia hali walipolazwa katika hospitali ya taifa Muhimbili (MNH) wanamuziki hao waliopata kutamba walilazwa hospitalini hapo baada ya kuugua kwa muda mrefu, kwa moyo wa kizalendo rais wa nchi aliguswa na kwenda kuwajulia hali.

Ameacha mambo mangapi Ikulu, inawezekana Kikwete ameonyesha kuguswa kuliko hata baadhi ya ndugu wa wanamuziki hao ambao huenda hawakuwahi kwenda kuwatazama, ni ujasili mkubwa unaoonyeshwa na rais kushirikiana na wasanii na wanamichezo.

Kikwete ni mwanamichezo shupavu ambapo alipoingia madarakani aliweza kutembelea mataifa mbalimbali duniani na kukutana na wachezaji wa vilabu tofauti na vikubwa kama Real Madrid, Barcelona na nyinginezo.

Ushirikiano wake tumeshuhudia Tanzania ikipata uenyeji wa ziara za kombe la dunia, pia timu za taifa hasa zile kubwa kisoka zilitembelea Tanzania, mbali na hilo muda ujao Real Madrid inafanya ziara nchini ambapo tutawashuhudia mastaa kama Gareth Bale na Cristiano Ronaldo.

Ukiondoa nyota hao wa Real Madrid, wakongwe Zinedine Zidane 'Zizzou', Ronaldo De Lima, Robert Carlos, Ruud Van Nisterooy na Luis Figo nao watatua, hizo zote ni jitihada za rais Kikwete na kuchangia kuitangaza Tanzania kiutalii.

Katika utawala wake tumeona viongozi mbalimbali duniani wakiitembelea Tanzania na kuvutiwa nayo, ziara kubwa ni ile ya rais wa Marekani Barack Obama aliyoifanya mwaka jana, Obama aliwasili nchini na familia yake.

Anawajali huyu! rais Kikwete alipokwenda katikia msiba wa marehemu Mzee Small nyumbani kwake Tabata Kimanga hivi karibuni.

Kikwete aliendeleza ukarimu wake kwa kujumuika pamoja na Watanzania wakati wa matatizo hasa misiba, hivi karibuni aliungana na waombolozeaji wengine katika misiba mfululizo hasa wa wasanii, JK alianzia msiba wa Muhidini Gurumo.

Na alipokuwa nje ya nchi, wasanii watatu waliaga dunia kwa mpigo, alianza Amina Ngaluma, Adam Kuambiana na Rachel Haule 'Recho' lakini JK aliipa hadhi misiba hiyo kwa kuzikwa kiserikali, katika misiba hiyo viongozi wa ngazi za juu wa serikali waliongoza mamia kuwazika ndugu zetu hao.

Katika utawala wake tumeshuhudia JK akiwaalika wasanii Ikulu, haikuwahi kwa wasanii wa hapa nchini kutembelea Ikulu zaidi ya hayati Michael Jackson 'The Jacko' ambaye ni marehemu, Jackson alialikwa na rais wa awamu ya pili Alhaj Alli Hassan Mwinyi.

Vilevile Kikwete alionyesha kukerwa na kitendo cha mmiliki wa timu ya TP Mazembe ya DRC- Congo Moitse Katumbi kuwazuia wachezaji wake Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wasirejee nyumbani kuitumikia timu ya taifa ambayo ilikuwa na mechi ngumu na muhimu ya kufuzu kwenye makundi ya michuano ya mataifa Afrika itakayofanyika Morocco.

Kikwete alipofanya ziara ya kikazi nchini DRC- Congo alitumia nafasi hiyo kuwatembelea TP Mazembe waliokuwa hotelini Lubumbashi na kukutana na Samatta na Ulimwengu.

JK kushoto akiwa na mwanamuziki wa kizazi kipya Diamond Platinum nchini Marekani walipokutana katika ziara zao.

 Pia alikutana na bilionea wa TP Mazembe Moitse Katumbi na kuzungumza naye kiundani na kumweleza umuhimu wa akina Samatta katika timu ya taifa ya Tanzania, haikuchukua muda nyota hao walipewa ruhusa na kurejea nyumbani na kuungana na wenzao kwenye kambi ya timu ya taifa.

Uwepo wao kwenye timu ya taifa uliisaidia kuiondoa mashindanoni Zimbabwe baada ya kufungana 2-2, katika mchezo wa kwanza Stars ilishinda bao 1-0, umuhimu wa Ulimwengu ulijidhihirisha ambapo yeye ndiye aliyeifungia Stars goli la pili.

Kikwete amewafanya wasanii wa Tanzania kutembea kifua mbele, hivi karibuni alienda katika msiba wa msanii mkongwe Mzee Small kisha kutembelea nyumbani kwa aliyekuwa katibu mkuu wa zamani wa chama cha soka nchini FAT sasa TFF Hassan Mwanakatwe ambaye alifariki sambamba na Mzee Small.

Huyo ndiye rais Jakaya Kikwete ambaye atanitoa machozi siku atakapoondoka madarakani.