come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

WAMBURA AWAKEBEHI WALIOMPINGA TFF

SIKIA hii: Mgombea wa nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu wa Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam, Michael Wambura, amesema baada ya kurejeshwa katika mchakato huo hana 'kinyongo' na wanachama waliokuwa wamemwekea pingamizi kwa sababu walikuwa na haki yao kufanya hivyo kwa mujibu wa katiba.


Wambura alisema pia kuanzia juzi yeye ni mgombea halali kuelekea uchaguzi huo utakaofanyika Juni 29, mwaka huu kwa sababu kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maamuzi ya Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya shirikisho hilo ni ya mwisho.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Wambura alisema kushinda kwa rufaa yake ni ushindi wa Wanasimba wote na itatoa fursa kwa wasioijua katiba kuisoma na kuifahamu vema.

Katibu Mkuu huyo wa zamani wa FAT sasa TFF, alisema uchaguzi huo usiwe ni sehemu ya kuwagawa wanachama wa Simba na kuongeza kuwa imefika wakati demokrasia iachwe ichukue nafasi yake kwa sababu wote wanataka kuijenga klabu hiyo.

Wambura alisema bado kuna safari ndefu kuelekea katika uchaguzi huo wa Simba na anawataka wanachama kusimama pamoja kuhakikisha wanaleta mabadiliko.

"Naomba walionipinga muwaone hawana hatia, ni Simba wenzenu hata kama walikuwa na nia na malengo binafsi au wametumwa," alisema Wambura. Alieleza kwamba yeye hakatai kufanya kazi na wafadhili ila Simba inahitaji wadhamini ili iweze kujiendeleza.

"Mfadhili anatoa fedha pale anapojisikia, na ukiruhusu wafadhili, ndiyo wajanja wachache wataingia," Wambura aliongeza.

Pia mgombea huyo alisema kuwa anashangaa kuona viongozi wanauza mchezaji tegemeo katikati ya msimu na wakati huo huo wanamalengo ya kufanya vizuri jambo lisilowezekana kamwe.

WANACHAMA WATOFAUTIANA
Baada ya juzi Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF kutangaza kumrejesha mgombea huyo kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi, wanachama wa klabu hiyo wametofautiana na maamuzi hayo.

Akizungumza jana jijini, Mohammed Wandwi mwenye kadi namba 5175 alisema kuwa yeye anawasiwasi timu yao haitafanya vizuri kwa sababu wajumbe waliopiga kura za kumrejesha kwenye mchakato wanatoka timu pinzani.

Ras Simba (5757) alisema kuwa kurejea kwa Wambura kumetokana na shinikizo kutoka kwa Kiongozi wa TFF na pia anashangaa kuona mgombea huyo anaungwa mkono zaidi na viongozi wa Yanga. "Hii ni hatari kwa Simba, hivi akishinda katika uchaguzi, Yanga watanufaikaje?", alihoji mwanachama huyo.

Alisema pia hata katika vikao vyake vya kupanga mikakati mgombea huyo anadaiwa kufanya pamoja na (alitaja jina la Rais wa zamani wa Yanga).

Naye, Boss Matola, alisema amefurahi kuona Wambura amerejeshwa katika mchakato huo wa uchaguzi na kwamba inaonyesha wazi haki imetendeka. Matola alisema kwamba anaamini Wambura ni mtu sahihi na atakayewaletea mafanikio wanayoyahitaji.

Juzi Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF ilitangaza rasmi kumrejesha Wambura kugombea Urais wa Simba na kubatilisha maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo.

Hata hivyo, Wambura anatarajiwa kujadiliwa tena kati ya leo na kesho  katika Kamati ya Maadili kutokana na mwanachama wa Simba, Jackson Sagonge 'Chacha' kuwasilisha malalamiko yake katika kamati hiyo tangu wiki iliyopita.

Kamati hiyo ndiyo ilimuengua Wambura katika uchaguzi wa TFF ikieleza kuwa si muadilifu na mwajibikaji.