Wakati wagombea nane wakienguliwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Simba, mchakato huo huenda ukasimama muda wowote kuanzia sasa kutokana na Kamati ya Uchaguzi ya Simba kukabiliwa na ukata.
Habari za uhakika ambazo gazeti hili limezipata zinadai wagombea ambao wameenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho baadhi yao ni wajumbe kamati zilizomaliza muda wake.
Pia, baadhi ya wagombea wengine vyeti vyao wameghishiwa na juzi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), walichukua vielelezo vya wagombea kwa ajili ya kuvichunguza.
“Hatuwezi kuendelea na mchakato wa uchaguzi hadi Takukuru wamalize uchunguzi wao, ila tambua tuna wagombea wengi hawana sifa ya uzoefu wa miaka mitatu na wengine vyeti vyao ni batili, wapo waliojiondoa mapema ila kuna wabishi ambao kamati itawashughulikia,” kiliongeza chanzo hicho.
Kuhusu fedha ambazo wanazitumia kuendesha uchaguzi huo kufikia ukingoni na tayari wameshautaarifu uongozi wa Simba kusitisha kuendelea na mchakato huo hadi wapate fedha za kuendeshea.
“Mchakato mzima unagharimu Sh29 milioni, fedha za kuuza fomu kwa wagombea zilipatikana Sh9.6 milioni, ndio zilizokuwa zinatumika na zimefikia ukingoni, muda wowote kuanzia sasa kamati inaweza kutangaza kusimamisha kwa muda mchakato huo,” kiliongeza.
Akizungumzia hali hiyo, Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alikiri kamati hiyo kukabiliwa na ukata na kudai wameshawasilisha suala hilo kwa wadhamini wao Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), ambayo imekuwa ikidhamini Sh20 milioni kila mkutano wa klabu hiyo.
“Tumeshawataarifu TBL juu ya jambo hilo, kwa kawaida huwa wanatoa fedha wiki mbili au mwezi mmoja kabla ya mkutano, lakini kutokana na hali mbaya ya fedha inayoikabili Simba ingekuwa ni hatari tuchukue fedha hizo mapema tulihofia kuziingiza kwenye usajili.
“Lakini tumeshaongea nao na Juni Mosi (kesho) wametuahidi watatuingizia fedha hizo na tutazikabidhi kwa kamati ili waweze kuendelea na uchaguzi,” alisema Kamwaga.
Hata hivyo, kamati hiyo inatarajiwa kuweka wazi majina ya wagombea walioenguliwa katika kinyang’anyiro hicho kesho.