MCHEZAJI nyota wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Mrisho Ngassa amesema wanaweza kuitoa Msumbiji na kufuzu kuingia kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco iwapo watakuwa na maandalizi mazuri kabla ya mchezo huo.
Akizungumza jana mjini hapa kabla ya kikosi cha Tanzania, Taifa Stars kusafiri kurejea Dar es Salaam baada ya kuitoa Zimbabwe juzi, Ngassa alisema kuitoa Mambas ni jambo ambalo linawezekana kama timu itapata maandalizi mazuri.
“Kama umeweza kuitoa Zimbabwe kwa nini ushindwe kwa Msumbiji, wote ni wale wale tu, hawapishani sana viwango vyao na ninadhani Zimbabwe wako juu zaidi ya Msumbiji,”.
“Cha muhimu hapa maandalizi tu, timu iingie kambini mapema, tufanye mazoezi na tupate mechi za kujipima nguvu ili kocha aangalie maendeleo ya timu na wachezaji,”alisema mshabuliaji huyo wa Yanga SC ya Dar es Salaam.
Taifa Stars itamenyana na Msumbiji katika hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kupangwa kwenye makundi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco baada ya kuitoa Zimbabwe juzi kwa jumla ya mabao 3-2, ikianza kwa ushindi wa 1-0 nyumbani na kumaliza kwa sare ya 2-2 juzi mjini hapa.
Mechi yake kwanza itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Julai 19 na 20 mwaka huu, wakati mechi ya marudiano itafanyika Msumbiji kati ya Agosti 2 na 3 mwaka huu.