Uongozi wa Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam umesema kwamba unatarajia kuandaa maandamano ya wanachama wake kwa mara nyingine yenye lengo la kushinikiza wapatiwe eneo la kujenga uwanja wa kisasa wa klabu hiyo.
Akizungumza juzi katika mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga, alisema kuwa bado nia ya wao kuandamana haijafa na wanaamini maandamano hayo yatasaidia kufanikisha maombi yao yanafanyiwa kazi.
Sanga alisema kuwa Yanga ni taasisi kubwa na ili kuiendeleza wanahitaji kujenga uwanja katika eneo hilo la Jangwani kwenye asili ya klabu yao na si mahali pengine.
Alisema kwamba licha ya mchakato huo kutumia zaidi ya miezi 19 na bado haujafanikiwa, hawatachoka kuendelea kukumbusha maombi yao na wanaamini uwanja utakapojengwa, kizazi kijacho cha Yanga kitanufaika na ujenzi huo.
Kiongozi huyo alieleza kuwa tayari wameshakubaliwa maombi yao kutoka kwa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam na sasa kikwazo kimebaki kwa ngazi ya Manispaa ya Ilala.
“Nguvu ya wanachama juu ya maombi ya eneo itaonekana zaidi katika maandamano, hii si ya sisi viongozi bali ni maombi ya Wana-Yanga wote,” alisema kiongozi huyo.
Alieleza kuwa kwamba Yanga inaendelea na msimamo wake wa kukataa udhamini wa kituo cha televisheni cha Azam kilichoingia mkataba na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Alisema kwamba wao wanachopinga ni kuona katika udhamini huo timu zote zinapata kiasi cha fedha sawa na timu nyingine wakati wao wana mashabiki wengi zaidi.
"Haiwezekani klabu ipande daraja leo na kupewa fedha sawa na Yanga, hii sikubaliani nayo, bora turuhusiwe kwenda (alitaja jina la kituo kingine cha televisheni)," aliongeza kiongozi huyo.
Kufuatia kugomea udhamini huo, Yanga ilikataa pia mechi zake za nyumbani zisirishwe hewani na kituo hiko.