Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania (FAT) Said El Maamry amesema alipenda rais aliyemaliza muda wake TFF, Leodegar Tenga kuendelea kuongoza shirikisho hilo kwa vile alilifikisha mbali.
Akizungumza na gazeti hili, El Maamry ambaye pia ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) alisema Tenga alipokea chama kikiwa kimegubikwa na migogoro, lakini alifanikiwa kuiondoa na kuliongoza shirikisho hilo kwa misingi ya uwazi.
“Binafsi sikupenda Tenga ang’atuke nilitaka aendelee. Nina uhakika angelipeleka soka letu mbali zaidi, (rais wa sasa, Jamal) Malinzi anatakiwa kuhakikisha viatu vya Tenga vinamtosha. Awe na mapenzi na mpira na asitumie mpira kama njia ya kusaka vyeo vya kisiasa,” alisema El Maamry.
“Anatakiwa awe mwaminifu katika mchezo wa mpira, uwazi katika masuala ya fedha na asiwe mchonganishi kwa pande zinazotofautiana bali awe mpatanishi, na ajue katiba zote za mpira wa miguu za CAF, Fifa, TFF, Mikoa na Wilaya.
“Apende wachezaji, mapenzi yake yasibague ajijue yeye ni kiongozi wa taifa na siyo kiongozi wa klabu, hivyo anapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa.”