NYOTA wa Brazil, Neymar Jr amefichua siri kuwa alishindwa kuzuia machozi na alikaribia kuwa kichaa baada ya kugongwa na Juan Zuniga na kuvunjika mfupa wa uti wa mgongo.
Neymar kwa mara ya kwanza alifanya mkutano na waandishi wa habari baada ya kutoka Hospitalini ambapo anauguza majeraha yake ya mfupa wa uti wa mgongo uliovunjika kwenye mechi ya robo fainali ya kombe la dunia dhidi ya Colombia.
Pia Neymar hajakubaliana na maneno ya wakala wake aliyemuita Luiz Felipe Scolari kuwa ni kocha mbaya, mwenye majivuno na aliyepitwa na wakati.
Hii inatokana na kitendo cha Brazil kufungwa mabao 7-1 dhidi ya Ujerumani katika mchezo wa nusu fainali ya kombe la dunia, jumanne ya wiki hii.
Mshambuliaji huyo mwenye miaka 22 ameweka wazi kuwa beki wa Colombia, Juan Zuniga ambaye alimgonga na goti kwenye uti wa mgongo alimpigia simu na kuomba radhi kwa kitendo hicho kilichomfanya asicheze tena michuano hii mikubwa duniani.
Neymar jana alitembelea kambi ya mazoezi ya timu ya Taifa ya Brazil iliyopo mjini Teresopolis na aliwasalimia wachezaji wenzake.
Pia ataambatana na wenzake hapo kesho katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu dhidi ya timu ya taifa ya Uholanzi.
Jumapili katika dimba la Maracana, mjini Rio di Janeiro, Argentina itacheza mechi ya fainali dhidi ya Ujerumani.
Kwaheri: Neymar aliweza kutabasamu wakati akiondoka kwenye mkutano wa kwanza na waandishi wa Brazil tangu apate majeruhi.
Amani: Neymar alikiri kuwa Zuniga amempigia simu na kumuomba radhi kwa kitendo alichomfanyia na kumaliza ndoto zake za kucheza kombe la dunia