come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: ANDREW COUTINHO: AKITUMIKA KAMA KIUNGO MSHAMBULIAJI WAPINZANI WATAISOMA NAMBA

Na Fikiri Salum

MAANDALIZI ya kushiriki michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati yameanza takribani wiki mbili sasa katika uwanja wa Bandari na fukwe za Coco jijini Dar es Salaam.


Mabingwa wa kihistoria Yanga wakiwa chini ya kocha mwenye hamasa kubwa Mrazil Marcio Maximo wanaendelea kujifua vikali, gumzo kubwa katika mazoezi hayo ni Mbrazil mwingine ambaye anacheza nafasi ya kiungo mshambuliaji Andrew Coutinho.

Mashabiki wengi wanaojitokeza kushuhudia mazoezi hayo wamekuwa wakimtazama vizuri Mbrazil huyo ambaye amekuwa akionyesha uwezo mkubwa anapokaa na mpira na kutulia nao kisha anatoa pasi nzuri kwa mwenzie.

Coutinho amekuwa akiwatisha mashabiki wa Simba ambao nao wamekuwa wakitazama mazoezi ya Yanga ili kumjua uwezo wake, wengi wao ambao ni mashabiki wa Simba wameukubali uwezo wake na wanasema Coutinho anahitaji mtu kama Boban au Chuji ili aweze kumtuliza.

Lakini ukimwekea mtu wa kawaida kama chipukizi Said Ndemla, Awadh Juma au Jonas Mkude hawana uwezo wa kumdhibiti, kiwango cha Coutinho ni cha juu na amekuwa akipiga mashuti ya kushtukiza.

Si mchezaji wa kubeza hata kidogo licha ya timu ya taifa ya Brazil kupigwa mabao 7-1 ilipocheza na Ujerumani, lakini uwezo wake binafsi ni mkubwa na amekuwa akitoa ushirikiano kwa wenzake.

Mwandishi wa makala hii alifanya mazungumzo binafsi na mchezaji huyo ambaye anazungumza Kireno lugha ya Wabrazil wote, Brazil ilitawaliwa na Ureno na ndio maana lugha yao ni Kireno.

Coutinho alisema yeye ni mchezaji kama wengine hivyo anastahili kujituma awapo uwanjani, anakiri Yanga ni timu kubwa baada ya kuona idadi kubwa ya mashabiki wanaokwenda kuwatazama, amedai nahofia sana presha ya mashabiki.

Lakini akadai aogopi wingi wao na anachofahamu ni kazi moja, Coutinho anapogusa mpira hushangiliwa kwa nguvu ila yeye anaona hizo ni kama changamoto kwake na wala avimbi kichwa.

Kwa jinsi anavyoweza kuuchezea mpira na kutoa pasi kwa ustadi mkubwa huku akipiga mashuti makali ya kushtukiza anafaa kucheza nafasi ya ushambuliaji au kiungo wa katikati.

Ni mzuri kama Haruna Niyonzima au kuzidi, anajua kuutuliza mpira na kupiga pasi fupi fupi hata ndefu, pia anakontroo safi na kupiga chenga za maudhi, ana kasi na mashuti ya kushtukiza.

Endapo anapangwa na Jerry Tegete basi Yanga itatisha sana kupitia upande wao, si legelege kama Wazungu wengine yeye ni shupavu na anajua soka la Kiafrika, ingawa hajawahi kucheza Afrika.

Lakini katika vilabu alivyopata kucheza ameshakutana na Waafrika wengi hivyo anawajua vilivyo, ni mchezaji mwenye nguvu za ajabu kwani kumnyang'anya mpira mbele yake utumie akili ya ziada.

Ni mjanja kwa mipira ya kuotea kwa kifupi ni bonge la mchezaji na na ndio maana mashabiki wa Yanga hawazungumzi kitu kuhusu yeye, hakuna mashabiki wakorofi kama wa Yanga lakini wako kimya kwa sababu jamaa anaweza.

Nilipomuuliza katika kikosi cha Yanga mchezaji gani anayekuvutia, akacheka akasema wote wanamvutia, nikamtajia mastraika wa Yanga ambao bado hawajatua kama Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza akadai uwezo wa mchezaji huko uwanjani na si nje ya uwanja.

Coutinho amewataka Okwi na Kiiza waje uwanjani harafu ndio hatajulikana nani mkali zaidi ya mwenzie, Coutinho amesema yeye ni kiungo wa kati lakini anaweza kucheza kama mshambuliaji.

Amejipa matumaini ya kung'ara katika michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati inayotarajia kuanza hivi karibuni nchini Rwanda, Yanga SC inatarajiwa kuingia kambini Bagamoyo wakati wowote kwa maandalizi zaidi ya michuano hiyo, ambayo wamepangwa kundi A pamoja na wenyeji, Rayon Sport, KMKM ya Zanzibar, Coffee ya Ethiopia na Atlabara ya Sudan Kusini.

Lakini pia ametamba kung'ara katika ligi kuu ya bara endapo tu mwalimu atampanga katika kikosi chake cha kwanza, Coutinho ameelezea kusikitishwa kwake na matokeo ya Brazil katika kombe la dunia.

Kung'ara kwa Brazil kuliwapa heshima Wabrazil wote duniani na kila wanapokwenda huogopewa, na kufedheheshwa kwa taifa hilo katika fainali za kombe la dunia zilizofanyika nchini kwao kumewadhalaulisha Wabrazil wote duniani, kila wanapokwenda wanaonekana hawafai tena.
Ila  amedai ndio mchezo wa soka ulivyo, kwani licha ya matokeo hayo bado Brazil inabakia kileleni kwa kutwaa mataji mengi ya kombe la dunia, Brazil imetwaa mara 5 huku Ujerumani na Italia mara 4 kila mmoja.

Huyo ndiye Andrew Coutinho Mbrazil wa Yanga ambaye anategemewa kuiongoza timu hiyo katika ligi kuu ya bara na michuano ya kimataifa mwakani, je atafanya maajabu! tusubiri 0755 522216.