Wakati nyota wawili wa kimataifa wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wa klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wanawasili nchini kesho alfajiri kwa ajili ya mechi dhidi ya Msumbiji (Mambas), timu hiyo imetumia muda wake mwingi kujifua kulinda lango baada ya kuruhusu magoli 11 katika mechi nne zilizopita.
Baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Zimbabwe katika kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika 2015 jijini Dar es Salaam, Stars iliruhusu magoli mawili katika sare ya 2-2 ya mechi yao ya marudiano jijini Harare, kisha Stars ikalala 4-2 katika mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Botswana, ikachapwa 2-1 dhidi ya timu ya jeshi la Botswana kabla ya kulala tena 3-1 dhidi ya wanajeshi hao waliomaliza katika nafasi ya pili ya Ligi Kuu ya Botswana msimu uliopita.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana kutoka Tukuyu mkoani Mbeya kwenye kambi ya Taifa Stars, nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro' alisema kuwa kocha wa timu hiyo ameifanyia kazi safu ya ulinzi kwa muda mwingi baada ya kuonekana inafanya makosa mengi.
Cannavaro alisema kwamba kila mchezaji sasa amepewa eneo maalum la kulifanyia kazi na anaamini jambo hilo litawasaidia kuimarisha safu yao ya ulinzi.
Alisema kuwa mazoezi mengi wanayoyafanya yanaimarisha timu hiyo na anaamini watawapa raha Watanzania Jumapili.
"Naamini katika mechi ya Jumapili tutapunguza au tutaepuka kufanya makosa ili tuibuke na ushindi mnono, ni mechi ngumu lakini tutaendelea kukumbushana na kupangana ili kutoruhusu wapinzani kutawala mchezo," alisema beki huyo wa kati anayeichezea timu ya Yanga ya Tanzania Bara.
Aliongeza kuwa mashabiki wa soka nchini wasisite kwenda kuwashangilia ili kuwaongezea ari ya kufanya vyema katika mechi hiyo muhimu ya kwanza kabla ya kurudiana mjini Maputo Agosti 3 mwaka huu.
"Tunajua wazi kwamba tukipoteza mechi dhidi ya Msumbiji tutakuwa nje ya mashindano ya kimataifa kwa kipindi kirefu, hivyo ni mechi ya kupambana kwa asilimia 100," Cannavaro aliongeza.
Wakati huo huo, Afisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema kuwa Ulimwengu na Samata watawasili jijini kesho saa 12 asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Misri wakitokea Tunisia ambako timu yao ya TP Mazembe imeweka kambi kwa ajili ya mechi za Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Hata hivyo, TFF haijaweka wazi kiungo wa Stars, Mwinyi Kazimoto, anayecheza soka la kulipwa Qatar atawasili nchini lini kujiunga na kikosi hicho.
Stars inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro itarejea jijini Ijumaa ikitokea Tukuyu na mechi yake dhidi ya Mambas itachezeshwa na mwamuzi, Mahmoud Ashour kutoka Misri.