MSHAMBULIAJI wa Atletico Madrid, Radamel Falcao amekuwa nyota baab kubwa kujiunga timu mpya iliyopanda Ligi Kuu Ufaransa, maarufu kama Ligue 1, Monaco inayomwaga fedha kama upupu kusajili, baada ya kufaulu vipimo vya afya katika klabu hiyo.
Baada ya kuwanasa wachezaji wawili wa
Porto, Joao Moutinho na James Rodriguez kwa Pauni Milioni 60 wote
Ijumaa, Monaco inamwaga 'mpunga' tena kumsajili kwa miaka minne au
mitano nyota huyo wa Columbian, na kumsajili Ricardo Carvalho kwa
mkataba wa mwaka mmoja, ambao unatoa nafasi ya kuongeza mwaka mmoja.
Mkataba wa mchezaji huyo mwenye umri wa
miaka 27, Falcao unampa uhuru wa kuondoka katika mwaka wa kwanza wa
kuwapo katika klabu hiyo, limesema gazeti la AS la Hispania.
Wakala Jorge Mendes wa Falcao na mmiliki wa Monaco, Dmitry Rybolovlev watamalizana juu ya vipengele vingine katika makubalino.
Atletico, ambayo Falcao ameichezea kwa
misimu miwili akiifungia mabao 70 katika mechi 88, itapata zaidi ya
Pauni Milioni 50 katika mauzo ya mchezaji huyo.
Kipengele kimoja katika mkataba huo
ambacho kimefungwa ni mshahara na Falcao atakuwa anapata jumla ya Pauni
Milioni 8.5 kwa msimu baada ya kodi. Carvalho,
mwenye umri wa miaka 35, ambaye amemaliza mkataba wake Real Madrid
baada ya misimu mitatu atatua kama mchezaji huru Ufaranmsa.