KAMATI ya Usajili ya klabu ya Simba, imenyanyua mikono katika harakati zake za kusaka saini ya mshambuliaji wa Xuan Thanh Saigon ya Vietnam, Mganda Moses Oloya (Pichani), baada ya kushindwa dau lake.
Dau lililoibwaga Simba ni dola 90,000 za Marekani, huku Wekundu hao wa Msimbazi wakifikia dola 35, 000.
Wakati hali ikiwa hivyo, uvumi umezagaa kuwa mahasimu wao Yanga wamemnyakua kwa dau hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope, alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba wameshangazwa na msimamo wa mchezaji huyo kubadilika ghafla, wakati awali walikubaliana kumnasa kwa dau la dola 35,000.
Alisema baada ya Oloya kuhitaji dola 90,000 pia klabu yake ambayo bado ana mkataba nayo, inataka dola 50,000.
Pope alisema hawawezi kumsajili nyota huyo kwa sasa kutokana na kutokuwa na michuano ya kimataifa, kwani amehitaji fedha nyingi ikiwa ni nje ya makubaliano.
“Sisi tulizungumza naye Oloya mwenyewe akakubali kuja kucheza Simba na akasema yuko katika hatua za mwisho kuvunja mkataba wake, tunashangaa ghafla anataka fedha zaidi ya za awali, basi hatuna jinsi, yeye aende tu anakoona watamlipa fedha hizo,” alisema Pope.
Tulipomsaka Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Binkleb, kuzungumzia hilo, alisema hadi jana mchana walikuwa hawajasajili mchezaji yeyote kukamilisha nafasi ya tano ya wachezaji wa kigeni na kuwa, endapo watafanya hivyo itajulikana.
Yanga kwa sasa ina wachezaji wanne wa kimataifa ambao ni Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Mbuyu Twite na Hamis Kiiza.