MABINGWA wa soka mkoa wa Pwani, Kiluvya United, mwishoni mwa wiki waliitambia timu ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Ruvu Shooting, kwa mabao 2-1 katika mchezo wa kirafiki uliochezwa uwanja wa Mabatini Mlandizi wilayani Kibaha.
Katika mchezo huo uliokuwa na upinzani wa hali ya juu dakika zote 90, maafande wa Ruvu Shooting walikuwa wa kwanza kuzifumania nyavu za wapinzani wao dakika ya 38, kwa bao lililofungwa na Cosmas Abel kwa shuti.
Kuingia kwa bao hilo, kulionekana kama kuichokoza safu ya ushambuliaji ya Kiluvya United, lakini hata hivyo walinzi hao walikuwa makini kazuia mashambulizi, hivyo hadi mapumziko matokeo yalikuwa 1-0.
Ilikuwa ni dakika ya 80, pale mshambuliaji Shala Juma almaarufu kama ‘Okwi’ alipowainua mashabiki wa Kiluvya baada ya kupachika bao la kusawazisha, kabla ya Amani Benard, kuiua kabisa Shooting kwa bao la pili, dakika za lala salama.