Dar es Salaam. Juma Nyoso na Ramadhan Chombo wameutaka uongozi wa Simba kuwalipa kwanza haki zao kabla ya kufikiria uamuzi wa kuwatoa kwa mkopo kwenda klabu nyingine.
Katikati ya wiki hii, Simba ilitangaza kuwatoa kwa
mkopo kwenda klabu ya Ashanti iliyopanda daraja msimu huu, lakini hatua
hiyo pia ikifuata baada ya awali kusimamishwa kwa muda usiojulikana kwa
utovu wa nidhamu.
Wachezaji wamesema hawako tayari kuondoka Simba
kabla ya kulipwa malimbikizo yao ya mishahara na haki zingine
walizostahili kupata kama wachezaji wa Simba.
Wamesema ndani ya klabu hiyo, hakuna anayewajali
wala kuwasaidia kupata haki zao, hivyo wanakusudia kuandika barua
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kueleza malalamiko yao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Nyoso alisema
ameshangazwa na utaratibu wa Simba kumtoa kwa mkopo wakati klabu hiyo
ikifahamu fika kwamba haijamlipa mishahara yake. Nyoso alisema
wanachofanya viongozi wa Simba ni kuwaburuta na kuwanyima haki zao za
msingi na hawako tayari kuona hilo linatendeka.
“Binafsi siendi Ashanti. Nataka wamalize kunilipa
madeni yangu yote na kisha mimi ndiyo nitaamua wapi niende lakini siyo
kwa kupangiwa na klabu ya Simba,” alisema Nyoso.
“Sioni taabu kukatisha mkataba wangu. Sijaona
utaratibu wa kumtoa mchezaji kwa mkopo wakati anadai mishahara yake.
Nimeamua kwenda TFF kuwashtaki,” aliongeza.
Aidha, Nyoso aliongeza kuwa viongozi wa klabu hiyo
wamekuwa wakipigiwa simu na kushindwa kujibu na walipojaribu kwenda
ofisini viongozi hao wamekuwa wakirushiana mpira kila mara.
Nyoso, Maftah na Chombo wamesema wanaidai klabu
hiyo mishahara ya miezi miwili, na kwamba baadhi ambao hawakuwa
wamelipwa walilipwa pesa zao baada ya kudai sana.
Gazeti hili lilimtafuta katibu mkuu wa klabu hiyo
ambaye ndiye mwenye dhamana ya malipo kwa wachezaji lakini simu yake
ilikuwa ikiita bila majibu.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ezekiel
Kamwaga alisema ni vyema wachezaji hao wakawa na subira ili walipwe
fedha hizo kwa vile mwamuzi wa mwisho ni uongozi wa klabu.
Wakati huohuo, kiungo wa Yanga, Nizar Khalifan
yupo katika mazungumzo na uongozi wa klabu ili kumwongezea mkataba
mwingine baada ya kuridhika na kiwango alichoonyesha msimu uliopita.