Vyanzo vinasema Mwenyekiti wa Yanga SC, Alhaj Yussuf Mehboob Manji ameipa Kamati ya Mashindano ya klabu, inayohusika na masuala ya usajili pia, chini ya Mwenyekiti wake, Abdallah Ahmed Bin Kleb fungu la kutosha ambalo ‘piga ua’ litatosha kumlainisha Oloya abadilie uamuzi wake.
Aidha, inadaiwa tayari mazungumzo kati ya Yanga na Oloya yanaendelea na kuna makubaliano- kana kwamba mchezaji huyo mwenye kasi, nguvu na uwezo mkubwa wa kumiliki mpira amekubali kuwapuuza Simba SC.
Simba SC imetenga nafasi katika usajili wake wa wachezaji wa kigeni na ipo tayari kumsubiri Oloya hata hadi Januari baada ya makubaliano ya kimsingi.
Kiungo huyo mshambuliaji wa The Cranes, yaani ndege aina ya Korongo aliyezaliwa miaka 20 iliyopita anamaliza mkataba wake na Saigon Xuan Thanh ya Vietnam mwezi huu, Agosti na kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe aliwaahidi atakuja Septemba.
Kwa sababu hiyo, Simba imepanga kusajili wachezaji wanne wa kigeni ambao ni Waganda, kipa Abbel Dhaira, beki Joseph Owino na Warundi wawili, mmoja beki na mwingine mshambuliaji, Amisi Tambwe.
Sasa ni wakati wa mpambano wa watani, kuwania saini ya mchezaji huyo aliyekwenda Vietnam akitokea KCC ya kwao, aliyoichezea tangu 2009 hadi 2010.
Katika usajili wake, Yanga ina nafasi mbili za wachezaji wa kigeni, sasa ikiwa na watatu ambao ni beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima na mshambuliaji Didier Kavumbangu- wakati bado ipo kwenye mazungumzo na Mganda, Hamisi Kiiza aongeze Mkataba.
Wakati huo huo, habari zinasema, Yanga SC wana mpango wa kuleta kiungo mshambuliaji hodari kutoka Brazil.
Kwa sasa Hans Poppe amekwenda Ureno kushughulikia mpango mmoja mzuri kwa mustakabali wa klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, ambao amekuwa akiupigania kwa muda sasa na maendeleo yake ni mazuri.