come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

OKWI RUKSA YANGA IJUMAA.

Utata wa usajili wa mshambuliaji Emmanuel Okwi kuichezea Yanga au la unaweza kumalizwa keshokutwa, Ijumaa.

Uamuzi huo huenda ukakata mzizi wa fitina na kumaliza mzozo wa uhamisho huo ambapo kumsajili na kumtumia Okwi kunaweza kuitia hatiani, kuishusha daraja au hata kuilazimisha timu kulipa faini ya mamilioni ya shilingi.

Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuzingatia Sura ya VIII, Kifungu 24, 26 na 29 cha Kanuni za Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Inayosema klabu inaweza kuondolewa katika mashindano na kufungiwa miaka mitatu kushiriki michuano yote ya Afrika, pamoja na shirikisho la nchi husika pia litafungiwa miaka mitatu kwa kuruhusu kufanyika uhamisho na kutumika mchezaji mwenye matatizo.”


Habari ambazo gazeti hili limezipata jana zilieleza kuwa tayari Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), limeshafunga uchunguzi  kuhusu suala hilo na linaweza kutoa hukumu yake Ijumaa baada ya kukusanya vielelezo mbalimbali kutoka klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia, Simba na Shirikisho la Soka la Uganda (Fufa).

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Rage alisema jana kuwa tayari wameipa Fifa nakala za vielelezo mbalimbali vya ushahidi kuhusu mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa amesimamishwa na TFF na kuzuiwa kuitumikia Yanga hadi pale suala lake litakapopatiwa ufumbuzi.

“Juzi, Fifa kupitia ofisa wao, Laura Saint Nelly walitutumia nakala mbalimbali, moja inaonyesha kuwa Okwi alisaini mkataba mrefu na Etoile du Sahel ambao unamalizika 2016.

“Nyingine ni ile ya Fifa  iliyomruhusu Okwi achezee Villa kwa muda baada ya Fufa kumwombea kibali na nakala nyingine ni ile ya Etoile du Sahel ambayo imekiri bado haijatulipa (Simba) Dola 300,000 ambazo tunawadai.

“Klabu hiyo imejitetea kuwa imekwamishwa na Benki Kuu ya Tunisia kuhamisha fedha kule kuja kwetu na nyingine ni ile ya Simba SC ambayo tuliwaandikia Etoile tukiwaongezea muda wa kutulipa kutoka Februari mwaka jana hadi Novemba, lakini wameshindwa kufanya hivyo.

“Kwa mujibu wa maelezo ya Laura, vielelezo vyote muhimu walishavipata na tayari wameshafunga uchunguzi wao, hivyo ndani ya wiki hii huenda wakatoa hukumu yao,” alisema Rage.

Hata hivyo, Rage anaeleza kuwa hukumu inaweza kuwa pigo kwa watani zao, Yanga ambao wamemsajili mchezaji ambaye bado ana mkataba na klabu nyingine.

Kwa kosa hilo, Yanga wanaweza kulimwa faini au kushushwa daraja, pia Okwi atakabiliwa na adhabu ya kulipa faini na hata  kufungiwa.