HUWEZI kuamini jinsi mshambuliaji wa Yanga Jerryson John Tegete anavyoendelea kubaki katika kiwango chake kilekile tangia mwaka 2006 alipoanza kuchomoza kwenye medani ya soka.
Tegete ninayemjua mimi alianza kusifika katika kikosicha timu ya taifa Taifa Stars iliyokuwa chini yake Mbrazil Marcio Maximo, Maximo alipenda kumwita Tegete katika kikosi chake mara kwa mara huku wadau mbaloimbali wakimbeza.
Walimbeza Maximo kwa kumwita Tegete ambaye hakuwa na jina kama ilivyokuwa kwa nyota wengine,Kipindi hicho Tegete alikuwa akiichezea Makongo High School timu ya shuleni kwake.
Kiwango chake kiliwavutia wengi kiasi kwamba kocha wa timu ya taifa kipindi hicho Marcio Maximo alipenda kuwaita wachezaji chipukizi watano kuwemo katikia kikosi chake ili kujifunza pamoja na kaka zao.
Nakumbuka Tegete akiwa na wanafunzi wenzake walikuwa wakijifua na Stars, hapo ndipo Tegete alipoweza kuonekana, safari ya Stars kuelekea nchini Brazil kwa ziara ya mafunzo iliweza kumtambulisha kijana huyo.
Tegete aliondoka na Stars kuelekea Brazil ambapo timu ya taifa ilikuwa katika maandalizi ya kushiriki michuano ya mchujo ya mataifa Afrika ambapo ilipangwa kucheza na Senegar.
Hata hivyo Stars ilipoteza kwa kufungwa mabao 4-0, hapo ukawa mwanzo wa Tegete kuanza kuonekana katika kikosi cha Stars, kipigo cha Stars toka kwa Wasenegar kilisababisha kuvunjwa kwa kikosi chote ambapo sasa Maximo alianza kuwatumia chipukizi wake alioambatana nao nchini Brazil.
Jerry Tegete alianza kuichezea Stars kwa mara ya kwanza na msaada wake ulianza kuonekana, kwa mara ya kwanza Tegete aliweza kuichezea Stars na kuweza kung'ara, aliweza kuibuka mfungaji bora katika mechi mbili za mwisho ambazo hazikusaidia kuivusha Stars.
Tegete anakumbukwa jinsi alivyoifungia Stars mabao mawili kati ya manne Stars ilipocheza na Cape Verde, katika mchezo huo Stars ilishinda 4-2.
Hapo ndipo Tegete alipoonekana mchezaji muhimu, Tegete alisajiliwa na Yanga akitokea katika kikosi cha Stars,tofauti na wachezaji wengine ambao husajiliwa kutokea katika vilabu vya ligi kuu.
Tegete alisajiliwa na Yanga akiwa katika kambi ya timu ya taifa na wala hakuwa na timu yoyote ya ligi kuu, Simba hadi sasa wanamkumbuka Tegete, aliweza kuiliza zaidi ya mara tatu walipokutana.
Amekuwa shujaa wa Yanga pindi inapotoka kufanya vibaya, kiwango cha mchezaji huyo kinapanda na kushuka katikia siku za hivi karibuni, ingawa majeruhi yamechangia kumkwamisha lakini benchi nalo limesababisha asionekana.
Kocha mkuu wa Yanga Mholanzi Hans Van Der Pluijm ameshindwa kuamini baada ya kuona makali yake katika mchezo dhidi ya Rhino Rangers uliofanyika katika uwanja wa Ally Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Katika mchezo huo Yanga iliibuka na ushindi mabao 3-0 na kuzidi kuikimbilia Azam iliyo kileleni mwa msimamo wa ligi kuu bara, Pluijm alishangazwa na uwezo wa Tegete ambaye ndiye aliyefungua kitabu cha magoli.
Tegete ameonyesha uwezo mkubwa katika mchezo huo na kufanikiwa kuitoka mara kwa mara ngome ya Rhino Rangers, akizungumza na safu hii Jerry Tegete amesema kuwa ameanza rasmi kuonyesha makali yake.
Anasema kuwa alikuwa akisumbuliwa na goti ila kwa sasa yuko fiti na takuwa akifunga kila mechi endapo mwalimu atampa nafasi ya kuanza, 'Nina usongo na nyavu, nimecheza mechi chache sana lakini nina magoli sita tena nafukuzana na wanaowania ufungaji bora', alisikika.
Tegete mpaka sasa amecheza mechi sita na maefrunga magoli sita ina maana amefunga goli moja kila mechi, Tegete ni mshambuliaji bora katika dhama hizi kwani na ana uwezo mkubwa wa kutupia mipira nyavuni.
Sifa kubwa ya mshambuliaji yeyote yule duniani ni kufunga,
Tegete ana sifa zote anajua kucheka na nyavu hivyo ni mmoja kati ya washambuliaji mahiri kabisa nchini, hadi sasa nyota huyo analia na Maximo.'Kuondoka kwa Maximo kumechangia kushusha morali yangu kwani alipokuwepo aliweza kuniiita kwenye timu ya taifa kwa mara kwa mara, unajua kuwepo Stars kunaongeza morali ya mchezaji husika', analalamika Tegete mfungaji wa kwanza katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Rhino.
Ili safu ya Yanga ionekane kali basi mwalimu anapaswa kumuanzisha Tegete na Mrisho Ngasa, mapacha hao wamekuwa wakielewana tangia muda mrefu, hata katika mchezo dhidi ya Rhino Ngasa na Tegete walicheza vizuri.Pia ana maelewano mazuri na Didier Kavumbagu au Hamisi Kiiza huku pembeni wakiwepo Ngasa, Okwi au Msuva, akielezea ubingwa wa bara,Tegete amesema Yanga inaweza kutetea taji lake msimu huu.
'Unajua Yanga ni timu kubwa inajua kukwepa viunzi tofauti na Azam ambao ndio mara yao ya kwanza kuwania ubingwa wa bara, najua Azam watachemsha katika mechi zao zilizosalia, ila Yanga itafanya vizuri tu', aliongeza. 'Yanga ni timu yenye wachezaji bora kwa sasa hata nisipokuwepo mimi basi atakayekuwepo9 atafanya vizuri na ndio maana umeona nimecheza mechi sita na nimefunga magoli sita', huyo ndiye Jerry Tegete.