come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

TAIFA STARS INAPOTAFUTWA 'VICHOCHORONI'

Na Fikiri Salum

NIMESHANGAZWA na uteuzi wa japo kubwa la makocha 40 na shirikisho la kandanda nchini TFF, jopo hilo limekabidhiwa jukumu la kusaka vipaji kwa ajili ya kuunda kikosi imara cha timu ya taifa, Taifa Stars.

Imani kubwa waliyonayo mashabiki wa soka nchini kwa TFF ni kuona maandalizi kabambe ya kuandaa kikosi muhimu cha timu ya taifa itakayoweza kuwatoa kimasomaso Watanzania yanafanyika kwa uangalifu na weledi mkubwa.

TFF iliyoingia madarakani hivi karibuni ikiwa chini yake rais Jamal Emily Malinzi imewahakikishia wapenzi wa soka kuwa wataifikisha Tanzania kwenye fainali zijazo za mataifa Afrika zitakazofanyika mwakani, Malinzi aliahidi kuboresha mambo kadhaa yanayosababisha uduni katika maendeleo ya soka nchini.


Baada ya kuanza rasmi kuongoza TFF, Malinzi aliteua kamati mbalimbali ambazo atasaidiana nazo katika kuendeleza soka, pia alitangaza jopo la makocha wazawa wapatao 40 ambao watazunguka kona zote za nchi kusaka vipaji ambavyo vitakuja kuibeba Tanzania, uteuzi huo umeungwa mkono na wadau wa soka nchini hasa kuwemo kwa makocha wazoefu.

Kilio cha wapenzi wengi wa soka nchini ni kutohusishwa kwa makocha wazawa pamoja na wachezaji wa zamani walipata kutamba hapa nchini katika kutafuta suluhisho la upatikanaji wa timu ya taifa imara, miaka nenda rudi Tanzania imekuwa ikiitwa 'Kichwa cha mwendawazimu'.

TFF ilionyesha kwamba Tanzania inatumia wanamichezo wake wazawa katika kuendeleza soka, uteuzi huo pia uliungwa mkono na wachezaji wa zamani ambao waliiletea heshima kubwa nchi, bila shaka sote tuliamini mafanikio ya soka la Tanzania yatapatikana.

Wapo baadhi ya makocha walioteuliwa na TFF wanauzoefu mkubwa na taaluma hiyo, Taifa Stars imekuwa ikifundishwa na makocha wa kigeni na imeshindwa kufikia mafanikio ya miaka ya 80 ambapo timu hiyo ikiongozwa na kocha mzawa.

Katika miaka hiyo, Stars ilifanikiwa kufuzu fainali za mataifa Afrika ambazo zilifanyika nchini Nigeria, Joel Bendera ndiye aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, mpaka sasa rekodi yake hiyo haijavunjwa, kufanya vibaya kwa Stars kumepelekea malalamiko kadhaa kutoka kwa wadau wa soka nchini na hasa wakililaumu shirikisho la kandanda TFF.

Wadau wengi walitamani wazawa wapewe jukumu la kuinoa Stars pamoja na na zoezi la upatikanaji wa wachezaji, miaka nenda rudi kikosi cha timu ya taifa kinatokana na wachezaji wa Simba na Yanga.

Licha ya uongozi wa Leodegar Tenga kupiga hatua kadhaa katika kuendeleza soka nchini ikiwemo timu ya taifa, lakini ulishindwa kutengeneza kikosi madhibiti na kushuhudia tukipoteza mechi mbalimbali kwenye ardhi yetu wenyewe.

Muda wa utawala wa Tenga ulipomalizika, Jamal Malinzi alichukua nafasi ya kuliongoza shirikisho hilo, Malinzi ameweza kusikiliza kilio cha wapenda soka wengi nchini kwa kuwapa jukumu makocha wazawa ili kutengeneza kikosi imara cha timu ya taifa.

Baada ya kuteua jopo la makocha 40 watakaosaidiana na kocha mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars mdenmark Kim Poulsen ili kuandaa kikosi cha mafanikio, mwishoni mwa wiki iliyopita rais wa TFF Jamal Malinzi alitangaza mikakati ya jopo hilo la makocha aliowateua hivi karibuni.

Malinzi alisema jopo hilo litazunguka mikoani na kuteua kikosi cha wachezaji wasiopungua 60 watakaopatikana kwa mtindo wa mashindano maalum, mashindano hayo yanafanana na kombe la Taifa ambayo ilikuwepo katika miaka ya nyuma na kupelekea kupatikana kwa timu ya taifa imara.

Malinzi alifafanua kwamba jopo hilo litafanikisha upatikanaji wa wachezaji 60 ambao ni wale walioonyesha kiwango katika mashindano hayo maalum, aliongeza kuwa wachezaji hao 60 watachujwa na kubakia 30 ambao watawekwa kambini Tukuyu mkoani Mbeya.

Katika uwekezaji huo Malinzi alieleza kuwa jumla ya shilingi Mil 366 zitatumika ikiwemo kuigharamia kambi maalum ya kikosi hicho, aidha alidai kwamba wachezaji 30 wa timu ya taifa, Taifa Stars wataungana na wachezaji hao na kukaa pamoja katika kambi yao iliyopo Tukuyu Mbeya.

Nadhani hilo ndio suluhisho kamili la upatikanaji wa timu ya taifa inayohitajika na Watanzania kwa muda mrefu, Kwa utashi wangu Malinzi amechemka, kwa mtindo anaoutumia kwanza utaigharimu nchi, fedha nyingi zinazotolewa na wahisani na zile zinazotolewa na serikali kupitia wizara yake ya Habari, Utamaduni na michezo zitatumika vibaya.

Njia sahihi ya upatikanaji wa timu ya taifa itakayoweza kukata kiu ya Watanzania itatokana na ligi imara, kwa vyovyote TFF yenye dhamana ya kusimamia soka nchini ingepaswa kuboresha ligi kuu na madaraja mengine.

Kwanza ingeongeza timu zifikie 20 badala ya 14 zilizopo ligi ingepata ushindani na kujenga uwiano sawa na ligi nyingine zenye ushindani mkubwa kama vile ya Afrika Kusini, timu zikiwa 20 zitamfanya mchezaji mmoja kucheza mechi 38 katika msimu mmoja tofauti na sasa ambapo mchezaji mmoja nacheza mechi 26.

Pia TFF ingerejesha ligi daraja la nne, la tatu na mengineyo kila ngazi ya wilaya hadi mkoa, ligi zote zingechezwa kwa mtindo wa ligi  nyumbani na ugenini na si makundi kama ilivyo sasa.

Lengo ni kuleta ushindani kwa wachezaji ambao ni hazina kwa taifa, bila shaka jopo la makocha 40 linaloongozwa na wazawa lingetumia ligi hizo kunasa vipaji, TFF pia ingefufua michuano yake ya FA, kombe la Nyerere pamoja na Taifa Cup ikiwa na malengo ya kuongeza ushindani.

Hiyo ndio njia mbadala kuliko hii ya kusaka wachezaji wa 'uchochoroni' na kutumia mamilioni ya fedha katika kuunda timu ya taifa, kama wameshindwa wachezaji wa Simba na Yanga au Azam ambao wamepata uzoefu wa kutosha kucheza ligi na michuano ya kimataifa watawezaje hao wanaojaribiwa mara moja!

Mshauri mkuu wa Jamal Malinzi anapaswa kutumia nafasi hii kumshauri bosi wake huyo ili kufanyia kazi maoni yetu, hilo ndio jambo la msingi tena muhimu kwani enzi za akina Kitwana Manara, Maulidi Dilunga, Abdallah Kibadeni au Juma Pondamali 'Mensah' na Peter Tino ligi na kombe la  taifa zilitumika kuwapa uzoefu.

Nakumbuka enzi za utawala wake Muhidin Ndolanga FAT sasa TFF aliweza kusimamia vema uendeshaji wa ligi nchini, licha ya kukutana na changamoto mbalimbali ukiwemo ukosefu wa wafadhili tofauti na sasa ambapo wafadhili wapo wengi, kipindi hicho ligi daraja la kwanza sasa ligi kuu ilishirikisha timu 20 na ligi za madaraja mengine zilikuwepo.


Naweza kusema kipindi hicho cha Ndolanga ndio kilikuwa cha mwisho kwa wachezaji wa Kitanzania kutumia fulsa ya kucheza ligi yenye ushindani, uongozi uliofuatia ulipoteza misingi imara na kupelekea kufa kwa ligi za madaraja ya chini huku ligi kuu ikiwa na timu chache.

Huenda uongozi wake Jamal Malinzi unaweza kufufua misingi ya soka iliyokuwepo enzi hizo ila anahitaji muda zaidi kuweza kufikia zama hizo ikiwemo kukabiliana na changamoto zilizopo.