Kocha wa Simba, Zravok Logarusic amesema wachezaji wengi Tanzania, hawana elimu ya mpira, lakini ni wepesi wa kulewa sifa kwa kujiona ‘masupa staa’.
Akizungumza katika Makao Makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Msimbazi, Logarusic alisema mashabiki wamekuwa wakisifu na kuwapa umaarufu wachezaji wakiwa wameng’ara kwa mechi moja tu.
“Nilichogundua hapa Tanzania mchezaji akicheza vizuri kwenye mechi moja, mbili basi mashabiki wataanza kumpa ofa kwa kumnunulia gari, kumpa fedha, wachezaji wenu elimu ya darasani waliyonayo ni ndogo.
“Kwangu mimi staa ni yule anayecheza vizuri katika kila mchezo, Tanzania kuna vipaji, lakini hakuna wachezaji!” Mcrotia huyo aliongeza kuwa “Mchezaji ni yule anayeandaliwa kuanzia utoto, lakini hapa Ramadhani Singano, Haruna Chanongo, Amri Kiemba wamecheza michezo mitatu katika dakika 90 au 45 anashindwa kufunga goli, kutengeneza nafasi za kufunga, halafu unajiita na wewe mchezaji?”
“Kwa aina hii ya wachezaji mlionao mnategemea nini msiwe wa 116 kwenye viwango vya Fifa? Kwanza nimeshangaa Kenya ya 120 na Tanzania ikawa ya 116, wachezaji wanatakiwa wajue wajibu wao, wajitambue. Wawe na nidhamu ya mchezo na siyo kulewa sifa na kusubiri mechi za Yanga, Simba, Azam basi.
“Siyo wachezaji wa Simba tu, hii imeshajengeka hadi kwa timu nyingine. Wachezaji wote wa Tanzania kama mechi inahusisha timu nyingine wachezaji wanacheza viwango vibovu, lakini kama Simba inacheza na Yanga, au Azam basi wachezaji wa timu zote watacheza kwa kujituma.
“Hii yote inasababishwa na ufinyu wa elimu na nidhamu ya mpira, kwangu mimi kikosi cha kwanza kina wachezaji 16, ambao 11 wataanza na watano wataingia, ili upate kikosi cha kudumu kwangu lazima ufanye kazi.
“Mchezaji akibweteka atapoteza malengo, siwezi kusema juzi alicheza vizuri, kesho atafanya vizuri, au keshokutwa, tunatakiwa kuanza na kuiangalia zaidi leo hii ambayo tupo nayo, fanya kazi kwa bidii.”
Katika hatua nyingine Loga amekiri ligi ni ngumu kwa sasa kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo kwa timu mbalimbali na yeye yuko tayari kwa lolote.
“Nimeshinda michezo miwili kati ya mitano niliyocheza, si mbaya sana, ila kocha ‘must be hire and fire’ (kocha anaajiriwa kwa ajili ya kufukuzwa), nimeshazoea hili, nimeshazoea presha za mpira na ninazipenda.