
Mahakama yatoa ruhusa Yanukovich akamatwe
Waziri wa Serikali ya Mpito ya
Ukraine amesema kuwa anamsaka Rais wa zamani wa taifa hilo Viktor
Yanukovitch ili ashtakiwe kwa kuhusika katika mauaji ya halaiki.
Jana usiku Viktor alionekana akisafiri na walinzi wake Mashariki mwa taifa hilo lakini baada ya hapo hajulikani aliko.
Hayo yakiendelea wachunguzi wa Uingereza tayari wamefika Ukraine kuthibitisha ni nani aliyehusika katika umwagikaji wa damu wa Alhamisi ambako waandamanji kadhaa walipigwa risasi na kuauwa na watu wanaoshukiwa kuwa walenga shabaha wa serikali.
Kulingana na Waziri wa Maswala ya Usalama wa Nchini wa mpito walinzi wa Viktor Yanukovitch walitengana naye katika mji wa ufuoni wa Sevas-topol katika jimbo la Crimean.
Waziri huyo alisema kuwa Rais huyo wa zamani alienda mafichoni mnamo Ijumaa.
Alienda Mashariki kuelekea mji wa Kharkiv ambako alilala na kisha akaelekea Done-Tski, ambako alijaribu kuruka kwa ndege lakini akazuiliwa kufanya hivyo na walinzi wa mpakani.
Aliendesha gari usiku hadi Crimea, ambapo alisimama katika kituo kimoja cha kibiashara kabla ya kuelekea kwenye uwanja wa ndege wa Sevas-Topol.
Muda mfupi baadaye alitoweka na msafara wa magari matatu na kufikia sasa hajulikani aliko.
Mwandishi wa BBC aliyeko Kiev amesema kuwa wachunguzi wa Uingereza wametembelea barabara za mji wa Kiev na kushuhudia alama za risasi kwenye kuta za mijengo.
Wachunguzi hao walisema kuwa alama za risasi zimeweza kuonyesha ni wapi katika mijengo kadhaa hapo mjini walenga shabaha wa Serikali walitumia kuwapiga risasi waadmamanaji.
Wachunguzi hao Waingereza waliokuwa wakihojiwa katika kipindi kimoja cha televisheni cha BBC walikataa kueleza aliyewatuma kuendesha uchunguzi wao kuhusu aliyesababisha mauaji ya waandamanaji wakisema swala hilo kwa sasa ni nyeti mno.
Hata hivyo walisema ushahidi wanaokusanya utasaidia Serikali ya mpito kupanga mashtaka ya siku za usoni.