BEKI wa kushoto wa Yanga SC, Oscar Joshua na mshambuliaji wa timu hiyo, Hussein Javu wameanza mazoezi mepesi baada ya kupata nafuu maumivu yao.
Wawili hao walikuwa nje wakati Yanga SC ikipata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumapili wa mabao 2-1 dhidi ya Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hiyo ilifuatia Oscar kuumia katika mchezo uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar Yanga SC ikilala 2-0 Uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Javu kuumia mazoezini baada ya mchezo huo.
Daktari wa Yanga SC, Sufiani Juma ameuambia mtandao huu leo kwamba, wachezaji hao wameanza mazoezi mepesi leo baada ya kupata nafuu.
Sufiani amesema wawili hao wataendelea na programu hiyo kwa siku nne na baada ya hapo, Kocha Mkuu, Mbrazil Marcio Maximo ataamua mustakabali wao.
Yanga SC inatarajiwa kushuka tena dimbani Jumapili, kumenyana na JKT Ruvu ya Pwani katika mfululizo wa Ligi Kuu.
Ikiwa na pointi tatu ilizovuna katika mechi mbili, Yanga SC itakutana na JKT yenye pointi moja iliyovuna katika sare ya 0-0 na Mbeya City Uwanja wa Sokoine, Mbeya kabla ya kufungwa 2-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam Jumamosi.
Chanzo Bin Zuneiry Blog