Na Elias John, Lilongwe
Wakati kikosi cha timu ya Taifa, Taifa Stars, kiliwasili salama Malawi jana kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ya mchujo wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia za Urusi 2018, nyota wa timu hiyo wameahidi kuulinda kwa nguvu zote ushindi walioupata nyumbani.
Wakizungumza muda mfupi kabla ya kupanda ndege, wachezaji Mrisho Ngasa, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Ally Mustapha ‘Barthez’, wamesema kuwa wa naenda kupambana ili kuulinda ushindi wa magoli 2-0 walioupata Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa.
“Tunajua ugumu wa mchezo wa marudiano... lakini tunaenda tukiamini tunaweza tukaulinda ushindi wetu, tupo tayari kwa mapambano,” alisema nahodha wa kikosi hicho, Cannavaro.
Kwa upande wake, winga wa timu hiyo, Ngasa, alisema kuwa mchezo hautakuwa rahisi, lakini ni jukumu lao kama wachezaji kuhakikisha timu inasonga mebele.
Alisema kuwa hawajavimba kichwa kwa matokeo ya mchezo wa kwanza na wanaenda kufanya kazi.
“Kikubwa tunaomba Watanzania watuombee, na sisi kama wachezaji tunajua jukumu letu, tunaenda kupambana,” alisema nyota huyo wa klabu ya Free State ya Afrika Kusini.
Ulikuwa ni ushindi wa kwanza kwa Stars iliyocheza mechi 11 bila ya kushinda na ushindi wa kwanza katika mechi tatu chini ya kocha mzawa, Boniface Mkwasa, aliyepewa mkataba wa miezi 18, kufuatia kutimuliwa kwa Mholanzi Mart Nooij.
Mchezo huo wa marudiano utachezwa kwenye mji wa Lilongwe ambako Stars inahitaji kuepuka kipigo cha zaidi ya bao moja ili kusonga mbele