Bajeti ya Serikali ya 2013-14 imeipa kisogo sekta ya michezo baada ya kutenga kiasi kidogo cha fedha za miradi ya maendeleo katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.
Serikali imetenga kiasi cha Sh600 Milioni pekee
kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Habari, Utamaduni na Michezo kiasi
ambacho ni kidogo ukilinganisha na mahitaji halisi ya sekta zilizoko
katika wizara hiyo.
Katika bajeti ya 2013-14, Serikali imetenga jumla
ya Sh20.7 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ambayo ni mishahara
ya Wizara, asasi na matumizi mengineyo ya wizara.
Akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali
kuhusu makadirio ya mapato ya Serikali kwa mwaka 2013-14 mjini Dodoma
jana, Waziri wa Fedha, William Mgimwa alisema kabla ya nyongeza, bajeti
ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilikuwa Sh21.3
bilioni, lakini baada ya Serikali kupitia mashauriano na Kamati ya Bunge
ya Bajeti kwa mwaka wa fedha 2013-14, iliongeza Sh9 bilioni na kufanya
jumla ya bajeti nzima kuwa Sh30.3 bilioni.
Hata hivyo, kiasi hicho cha Sh9 bilioni
kilichoongezwa ni kwa ajili ya kuongeza usikivu wa Televisheni ya Taifa
(TBC), Sh6 bilioni na Mfuko wa Maendeleo wa Vijana Sh3 bilioni.
Katika mchanganuo huo, Serikali haijagusa kabisa
sekta ya michezo licha ya juzi Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na
Michezo, Amos Makalla kuitaka Serikali itenge kasma ya kutosha kwa ajili
ya timu za taifa za soka na klabu kwa kuwa zinawakilisha Tanzania
badala ya kutegemea Kamati za Ushindi.
Makala alisema: “Nadhani kuna haja ya kutenga
fedha hapa...linapokuja suala la timu za taifa ya soka au netiboli
tunakimbizana kuunda Kamati za ushindi, Kamati za kutafuta fedha, sawa
zinasaidia, lakini kwa nini kasma isitengwe?”
Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2012-13, Wizara
ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ilitengewa kiasi cha Sh3 bilioni
kwa ajili ya miradi ya maendeleo tofauti na bajeti ya mwaka huu wa
fedha 2013-14, ambapo kilitengwa kiasi cha Sh600 milioni pekee kwa ajili
ya miradi ya maendeleo.
Katika mwaka wa fedha wa 2012-13, Wizara ilitengewa Sh16 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida