come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAZOEZI YANGA NOMA, SASA KAMILI KUCHEZA KAGAME

JUMLA ya wachezaji 15 wa kikosi cha kwanza cha Yanga SC hadi jana walikuwa wameripoti mazoezini kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam kujiandaa na msimu mpya, wakiwemo wawili wapya Shaaban Kondo na Rajab Zahir, ambao walikuwa kwenye rada za wapinzani wao wa jadi, Simba SC.

Simba SC ilimuita mazoezini Kondo aliyekuwa anacheza Msumbiji na kufanya mazungumzo na Rajab, lakini kabla haijawasaini wachezaji hao, wapinzani wao Yanga SC wakawakamata ‘juu kwa juu’ na tayari wamejiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mbali na wachezaji hao wapya, wengine wanaoendelea na mazoezi chini ya kocha Mholanzi, Ernie Brandts ni Mrundi Didier Kavumbangu, Juma Abdul, Jerry Tegete, David Luhende, Ladislaus Mbogo, Salum Telela, Omega Seme, Said Bahanuz, Oscar Joshua na Nizar Khalfan pamoja na Yussuf Abdul, Joseph Banda na Rehani Kibingu waliopandishwa kutoka timu B.
Wachezaji wengine wa Yanga kwa sasa wapo na timu zao za taifa, kwa ajili ya mechi za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia, wakati wengine wamemaliza mikataba na inasemekana wametemwa.
Wanaodaiwa kutemwa ni Nsajigwa Shadrack, Godfrey Taita, Stefano Mwasyika, Said Mohamed na Nurdin Bakari, wakati Mrisho Ngassa, Simon Msuva, Ally Mustafa ‘Barthez’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’ na Frank Domayo wapo katika kikosi cha Taifa Stars na Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima wapo na Rwanda, Amavubi kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia. 
Yanga ipo katika maandalizi ya kwenda kutetea taji lake la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, michuano iliyopangwa kuanza Juni 18, mwaka huu nchini Sudan.
Hata hivyo, kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo, Yanga SC haijatoa msimamo wake rasmi juu ya kushiriki au kutoshiriki michuano hiyo.
Yanga wamepangwa Kundi C katika michuano hiyo pamoja na Ports ya Djibouti, Express ya Uganda na Vital 'O' ya Burundi, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC wamepangwa Kundi A pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman  ya Somalia na APR ya Rwanda.
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kufikia tamati Julai 2, mwaka huu mjini Khartoum, Sudan, mabingwa wa Kenya, Tusker wamepangwa Kundi B pamoja na wenyeji wengine, Al-Hilal, Falcons ya Zanzibar, Al Ahly Shandy ya Sudan na Al-Nasir Juba ya Sudan Kusini.
Yanga wataanza kampeni zao za kutetea taji hilo Juni 20 kwa kumenyana na Express, wakati Simba SC itashuka dimbani Juni 21 kufungua dimba na El-Mereikh, na mechi zote zitachezwa Elfashar.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga alisema wiki iliyopita kwamba kuwa ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika kwenye miji ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini nchini Sudan utategemea tamko la Serikali ambayo kwa sasa inafanya tathmini ya hali ya usalama.
“Masuala ya usalama yako nje ya uwezo wa CECAFA. Kwa hiyo, kama Serikali itabaini kuwa hali usalama ya huko si nzuri, hatutaziruhusu na kama ikiona hali ni nzuri, itaruhusu,” alisema Tenga.
“Jukumu la CECAFA (Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati) ni kuandaa mashindano na kupata uhakika wa usalama kutoka nchi mwenyeji.
“Kama tukipata uhakika huo wa usalama, mashindano yanafanyika. Lakini nchi moja moja zinayo haki ya kuhoji usalama kwa kuwa ni wajibu wa Serikali hizo kujali maisha ya wananchi wake.”
Tenga alisema kuwa mashindano hayo yalikuwa yafanyike Ethiopia, lakini katika dakika za mwisho nchi hiyo iliomba isiandae mashindano hayo hadi mwakani na ndipo Sudan ilipojitokeza kuokoa mashindano hayo.
Alisema wakati wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) uliofanyika Mauritius, CECAFA iliitisha mkutano mkuu wa dharura na kupewa taarifa ya maandalizi ya mashindano hayo kutoka uongozi wa Chama cha Soka Sudan na wanachama wakaridhia baada ya kuhakikishiwa usalama.
“Hivyo nchi wanachama wa CECAFA zimeridhia kushiriki baada ya kuhakikishiwa usalama, lakini kwa kuwa Waziri wetu (wa Mambo ya Nje, Bernard Membe), ameonyesha wasiwasi kuhusu usalama wa Darfur, hatuna la kufanya zaidi ya kumsikiliza. Ni kauli ya kiongozi anayeonekana kuwajibika na ni lazima tusubiri tamko la Serikali,” alisema Tenga.
“Lakini napenda kuishukuru Serikali ya Sudan kwa uamuzi huo kwa sababu kuandaa mashindano hayo si kitu kidogo. Tayari Katibu Mkuu wa CECAFA (Nicholas Musonye) ameshakwenda kwenye maeneo hayo na kukaa wiki nzima akikagua viwanja na hoteli zitakazotumika na kuridhika nazo,” alisema.
Alisema watu wasipotoshe tamko la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alilolitoa Bungeni kuhusu ushiriki wa timu zetu Darfur.
“Mhe. Membe alisema Serikali itafanya uchunguzi ijihakikishie kuwa hali ya usalama ni nzuri… alisema Serikali haitakubali kuruhusu raia wake kwenda Darfur wakati hali ya usalama si nzuri,” alisema Tenga.
“Kwa maana hiyo, na baada ya TFF kuipa Serikali taarifa zote muhimu kuhusu hali itakavyokuwa wakati wa mashindano, sasa tunasubiri tamko la Serikali. Na hii ni kawaida kabisa kwa kuwa hata hapa tunapoaandaa mashindano, ni lazima kwanza tupate uhakika wa usalama kutoka serikalini ndipo tuziite timu.”
Alifafanua kuwa si jukumu la CECAFA kuamua mashindano yafanyike mji gani na kwamba chama cha nchi mwenyeji ndicho kinachoamua mashindano yafanyike mji gani.
“Sasa kwa suala la Sudan, magavana wa majimbo hayo mawili ya Darfur Kaskazini na Gordofan Kusini waliomba kwa chama chao mashindano hayo yafanyike kwenye miji hiyo na Serikali ya Sudan ikaihakikishia CECAFA usalama,” alisema.
“Sasa ikitokea Serikali yetu ikasema hali si nzuri, hatutaziruhusu timu zetu ziende kwa sababu masuala ya usalama yako nje ya CECAFA,”alisema Tenga.