come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

HOME BOYS WAIBUKA WABABE MBELE YA MATHARE



Licha ya kusalia na wachezaji kumi, Kakamega Homeboyz walinyoa Mathare United 1-0 nyumbani kwao Bukhungu, Kakamega katika mechi ya Ligi Kuu Kenya Jumamosi.

Noah Abich aliibuka kama mwamuzi wa mechi hiyo baada ya kufanikiwa kufunga bao la pekee kupitia mkwaju wa penalti katika dakika ya 28 ya kipindi cha kwanza baada ya mlinda ngome wa zamani wa taifa, Edgar Ochieng, kumwangusha mshambuliaji Ronald Omino kwenye eneo la hatari.
Abich aligeuka kua tatizo pale alipolishwa kadi yake ya pili ya njano kwa kumfyeka kimakusudi Vincent Odongo hatua chache kutoka eneo la hatari.
Homeboyz walidhibiti mechi hiyo katika kipindi cha kwanza licha ya mechi hiyo kushuhudia machache huku kiungo wa zamani wa AFC Leopards, Bernard Ongoma, akionekana kwamba aliongeza uongozi wao katika dakika ya 35 lakini bao lake la kichwa kutoka krosi ya Daniel Waweru lilikataliwa kwani alikua ameotea.
Abich alipata njano yake ya kwanza kwa fauli dhidi ya Odongo huku Andrew Kulecho na Lloyd Wahome wakiungana naye katika kitabu cha adhabu baada ya Wahome kumchezea mshambuliaji wa Homeboyz, Allan Otindo katika dakika ya 42.
Dennis Nzomo aliwahi nafasi ya kwanza kwa timu ya Mathare pindi kipindi cha pili kilipoanza huku timu zote husika zikiimarisha harakati za kufunga.
Mchezaji wa timu ya nyumbani Dennis Mukaisi, nusura ajifunge na kusawazisha lakini Nyapala akaokoa kutoka utepe wa lango huku Mathare wakiongeza makali.
Abich aliaga mchezo katika dakika ya 71, tukio ambalo lilizua hisia tofauti kutoka mashabiki waliokerwa na uamuzi wa refa.
Mukaisi alipata fursa ya kuua mechi hiyo na goli la pili lakini mlinda lango wa Mathare, Peter Odhiambo, alizima jaribio lake hatua chache kutoka lango katika dakika ya 80.
Wenyeji wangempoteza Omino baada ya kugongana na Ochieng katika dakika za mwisho mwisho lakini alirejea baada ya matibabu ya muda.
Ijapokua Mathare walibobea katika kipindi hicho, hawakufanikiwa dua na wakasalimu amri kwa mara ya pili mfululizo katika Ligi huku wenyeji wakizoa alama zote tatu.