MKURUGENZI wa bendi muziki wa dansi ya Extra Bongo ‘Wazee wa Kizigo’, Ally Choki (Pichani), juzi alimtambulisha mwimbaji mpya wa bendi hiyo, mwanadada, Zena Muharami ‘Chinese’, akitokea bendi ya Victoria Saund.
Mbali na mwanadada huyo ambaye Choki alimtambulisha katika ukumbi wa Meeda Club ulioko Sinza jijini Dar es Salaam katika shoo yake ambayo inafanyika hapo kila Jumamosi, pia aliwatambulisha wanenguaji wawili, wakitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
“Naamini uwepo wa mwanadada huyu utazidi kuwapa raha mashabiki wa bendi hii, hivyo tunaomba sapoti kwa mashabiki wetu,” alisema Choki.
Mbali na utambulisho huo, Choki aliutambulisha wimbo mpya wa bendi hiyo unaojulikana kwa jina la ‘Mgeni’ ambao ulikonga nyoyo za mashabiki na kumfanya kila mmoja aamke katika kiti ambacho alikuwa amekikalia.
Choki alisema wimbo huo ni mfululizo wa kuwapa raha mashabiki wa bendi hiyo na kwamba bado kuna hazina kubwa ya nyimbo ambazo amepanga kuzitambulisha hivi karibuni.
Licha ya kutamba na kazi hizo, bendi hiyo inafanya vizuri na vibao vyake kama, ‘Mjini Mipango’ ‘Double double’ na nyingine ambazo zinafanya vizuri katika tasnia ya muziki wa dansi.