come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

NGASSA AELEKEZA NGUVU ZAKE YANGA

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mrisho Khalfan Ngassa (Pichani) amesema sasa anaelekeza nguvu zake katika kuisaidia klabu yake, Yanga SC kushinda mataji na kutawala soka ya nchini, baada ya timu ya taifa, Taifa Stars kutolewa kwenye Kombe la Dunia na CHAN.


Akizungumza kabla ya kuondoka mjini Kampala jana, Ngassa alisema alijitolea kila kitu ili kuisaidia timu ya taifa, lakini anaona bahati haikuwa yao na kwa kuwa soka ndiyo ajira yake, anasonga mbele.

“Tuko nje ya Kombe la Dunia na CHAN, tuna mechi ya kukamilisha Ratiba Kombe la Dunia na Gambia. Baada ya hapo biashara itaendelea na timu ya taifa na ninaamini bado nina nafasi kwa kocha na wananchi pia,”.

“Kwa sasa kwa kweli narudi nyumbani kupumzika kama siku mbili, kisha nijiunge na klabu yangu (Yanga SC). Sasa nataka kuisaidia Yanga, najua wapenzi kule wana hamu ya kuniona tena nachezea Yanga Uwanja wa Taifa. Na mimi nina wajibu wa kuwapa furaha. Nataka kuisaidia Yanga kushinda mataji,”alisema.

Ngassa alicheza vyema wakati Stars ikifungwa 3-1 na Uganda katika michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa wa Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.

Katika mchezo huo, uliofanyika Jumamosi, mtoto huyo wa kiungo wa zamani wa Simba SC, Khalfan Ngassa alitoa pasi ya bao pekee la Stars lililofungwa na Amri Kiemba wa Simba SC na akakaribia kufunga mara mbili, mara moja akigongesha mwamba na mara nyingine, akiikosakosa krosi ya Erasto Nyoni ndani ya sita.

Matokeo haya yanaifanya Tanzania itolewe kwa kufungwa jumla ya mabao 4-1, baada ya awali kufungwa 1-0 Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

Ngassa amesajiliwa Yanga SC majira haya ya joto akitokea kwa wapinzani wa jadi, Simba SC ambako alikuwa anacheza kwa mkopo akitokea Azam FC.

Hata hivyo, Simba SC inadai Ngassa waliingia naye Mkataba mpya baada ya kumaliza mkopo wake, hivyo baada ya kusajiliwa Yanga, inabidi walipwe dau la uhamisho wake.
Ngassa mwenyewe amekanusha kuingia Mkataba mpya, akidai alipewa fedha ili akubali kuichezea Simba SC kwa mkopo.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekwishatathmini hadhi ya mchezaji huyo na kusema ana Mkataba na Simba SC- maana yake, Yanga sasa wanatakiwa kumhamisha kutoka kwa watani wao hao wa jadi.

Tayari Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema wanataka si chini ya Sh. Milioni 100 kumuachia mchezaji huyo acheze kwa watani.