BONDIA Thomas Mashali (Pichani) amewafananisha mabondia wenzake, Mada Maugo na Kalama Nyilawila kama midoli kwa kuwakebehi kuwa hawana lolote ulingoni.
Mashali amefanya hivyo siku chache baada ya kupondwa na Maugo kwamba hana uwezo wa kupigana masumbwi, hivyo ni heri akatafuta kazi nyingine ya kufanya kama kuuza chapatti, huku Kalama akisema yeye ni mbabe wa Mashali.
Akizungumza katikati ya wiki hii wakati akifanya mazoezi katika gym yake Manzese, jijini Dar es Salaam, Mashali alisema Maugo na Kalama hawana uwezo wa kupambana naye kwani kwake ni kama midoli ya kuchezea watoto.
Mashali amejibu tambo hizo huku akikabiliwa na pambano dhidi ya Maugo litakalofanyika Oktoba 30 kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam kabla ya kumvaa Nyilawila.
“Kusema kweli huwezi ukanilinganisha na Maugo au Kalama… hawa kwangu ni kama midoli, hivyo hata maneno hayo wanayosema ni kujifariji, lakini ngoja tu siku itafika kila mmoja ataona hiki ninachokisema,” alisema Mashali huku akionesha midoli miwili mmoja akiwa Kalama na mwingine Maugo.
Alisema anaamini uwezo wake wa sasa utakuwa wa juu zaidi ya Maugo na Nyilawila licha ya kuwahi kutoka sare na Nyilawila.
Siku ya pambano la Oktoba 30, kutakuwa na mengine ya utangulizi kwa Ibrahim Class 'King Class Mawe' kuzichapa na Halid Manje katika raundi sita.
Aidha, kwa kila mpenzi na shabiki wa mchezo huo atakayefika ukumbini atapata fursa ya kununua DVD mpya za mafunzo ya mchezo wa masumbwi zitakazokuwa zikiuzwa na Rajabu Mhamila 'Super D' kwa bei ya kawaida ili kutoa nafasi kujifunza mbinu mbalimbali za mchezo huo.
DVD hizo mpya ni kati ya Mike Tyson dhidi ya Evander Holyfield na nyingine ni kati ya Felix Trinidad vs Roy Jones Jr; na Felix 'Tito' Trinidad vs Pernell Whitaker, ambazo zimerekodiwa kwenye kiwango bora.