MSANII mahiri wa muziki wa kizazi kipya, Tumaini Martin ‘Mwanakibibi’(Pichani) anatarajia kuachia filamu yake ya kwanza tangu arejee nchini kutoka Msumbiji alikokuwa akifanya shughuli za kimuziki.
Akizungumza jana, Matumaini alisema filamu hiyo itakayokwenda kwa jina la ‘The Dream’ ni yenye ubora wa kiwango cha Juu kimaudhui kutokana na aina ya wasanii walioshirikishwa.
“Hii ni filamu ambayo baada ya kutoka, naamini kila mmoja atavutika nayo kwani nimewashirikisha wasanii mahiri wakiwamo wa vichekesho kama Kiwewe, Mtanga, Bambo, Senga, Pembe, Njiwa, Gondo, Zimwi, Kombo, Chili, na wengine wengi,” alisema.
Alisema kutokana na ubora wa kazi hiyo, kila mpenzi wa burudani ataipenda, hivyo amewataka kukaa mkao wa kula kwani mambo mazuri hayataki haraka.
Ametoa nafasi pia kwa yeyote anayetaka kuisambaza ajitokeze kwake kwani lengo ni kuifikisha kazi hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.