Onyesho hilo litakaloambatana na burudani kutoka kwa wasanii wakali wa miondoko hiyo nchini litafanyika jijini Dar es Salaam likiambatana na maonyesho ya upakaji rangi na uchoraji, mitindo na mavazi pamoja na utoaji wa tuzo kwa wadau mbalimbali waliolisaidia kundi hilo lenye maskani yake Kinondoni, Dar es Salaam.
Kinara wa kundi hilo, Karama Masoud 'Kalapina', alisema maandalizi ya onyesho hilo lililokwama kufanyika Mei 31 kupisha msiba wa Albert Mangweha, yamekamilika na mgeni rasmi atakuwa Prof. Lipumba baada ya Mbunge wa Kinondoni, Idd Azan kuwaambia ana udhuru.
Kalapina aliwataka mashabiki wafike ukumbini kupata burudani ambayo hawajaipata kitambo kutokana na Kikosi kujipanga vyema wao na wasanii watakaowasindikiza.
Alisema wasanii watakaowasindikiza wakiwamo wakongwe na wengine wamejipanga kuwapa burudani na kuwaonyesha mizizi na utamaduni halisi wa Hip Hop.
"Burudani itakuwa ya kutosha kwa watakaofika kwani wasanii wa kikosi na wale watakaotusindikiza wamejipanga vyema, yaani mizinga 21 itapigwa kuadhimisha miaka 13 ya Kikosi," alisema Kalapina.
Baadhi ya wasanii watakawasindikiza Kikosi cha Mizinga ni Afande Sele, Young Killer, Kala Jeremiah, Mac 2 B, Mansu-Lee, Life With Purpose (LWP Majitu), Manzese Crew, Stereo, Nyandu Tozi, Gangwe Mobb na Inspekta Haroun na wakali wengine.