come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SIMBA YAWAZUIA WANACHAMA WAKE KUFANYA USAJILI


Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, 'Mzee Kinesi'
 
Uongozi wa Simba umesema hautaruhusu mwanachama yoyote wa klabu hiyo kusajili mchezaji kwa matakwa yake kwa ajili ya kuichezea timu hiyo.

Akizungumza na mtandao huu jana, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, 'Mzee Kinesi' alisema uongozi unakaribisha mwanachama yoyote wa klabu hiyo ambaye anataka kuisaidia kwenye usajili.

Lakini akaweka wazi kuwa hawataruhusu mwanachama huyo kusajili mwenyewe mchezaji bila kushirikisha benchi la ufundi na uongozi kwa ujumla."Kama uongozi tunakaribisha mwanachama yoyote kuisaidia klabu katika usajili," alisema Mzee Kinesi.

"Lakini hatutaki makundi (kikosini) na ndio maana tunasema hatutakubali mtu kusajili mchezaji wake mwenyewe na kumleta klabuni bila kamati ya usajili, benchi la ufundi na uongozi kwa ujumla kushirikishwa."

Palikuwa na tabia ya baadhi ya wanachama, hasa wanaojiita marafiki wa Simba, kuingia mikataba na wachezaji na kuwaingiza kikosini kwa ajili ya kuichezea timu hiyo.

Pale ambapo mwanachama huyo angekorofishana na uongozi, au kutonufaika na usajili aliofanya, ilitokea kuwa mchezaji husika alishawishiwa kuhujumu timu hivyo kupelekea Simba kufanya vibaya.

Alisema ikionekana mwanachama anataka kusajili mchezaji mwenyewe na kwa madhumuni yake binafsi hawatakuwa tayari kumpokea mchezaji huyo.

"Kipindi cha nyuma kulikuwepo na maneno mengi na mgawanyiko miongoni mwa wachezaji kwa sababu tu walitofautiana katika kusajiliwa," alisema na kueleza zaidi, "kwa sasa hatutaki suala hilo litokee na ndio maana hatutaki mtu binafsi kusajili mchezaji.

"Mwanachama kama anataka kuisaidia klabu anaweza kuleta fedha hizo za usajili kwa kamati husika na usajili utafanyika kulingana na matakwa ya klabu."

Kauli hiyo ya Mzee Kinesi imekuja siku mbili baada ya aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba Geofrey Nyange 'Kaburu' kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema hajaridhishwa na usajili wa baadhi ya nafasi ndani ya timu hiyo.

Kaburu alisema kama mwanachama hajaridhishwa na usajili hivyo yupo tayari kuisaidia timu hiyo katika zoezi hilo na Mzee Kinesi alisema wameisikia na wanaifanyia kazi kauli hiyo.

Simba inaendelea na maandalizi yake kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu chini ya kocha na gwiji wa zamani wa timu hiyo Abdallah 'King' Kibadeni