‘BRAZIL' inawezekana’ ndiyo kauli mbiu ya Taifa Stars leo watakaposhuka kwenye Uwanja wa Stade de Marrakech kupambana na wenyeji wao, Timu ya Taifa ya Morocco katika mchezo wa kusaka kufuzu kwa Kombe la Dunia 2014.
Stars wanashuka kwenye mchezo huo kwa lengo moja
la ushindi dhidi ya Morocco, huku wakiwa na kumbukumbu mbaya kwenye
uwanja huo waliponyukwa 3-1 mwaka 2011.
Matumaini ya Stars katika mchezo huo yatakuwa kwa
mshambuliaji wa TP Mazembe, Mbwana Samata ‘Samagol’ ambaye amefunga
mabao 13; Ligi ya Mabingwa mawili, Kombe la Shirikisho 2, Linafoot
(4) na mechi za kirafiki (5) akiwa na klabu yake mwaka huu, huku
akifungia Stars mabao mawili katika kampeni ya mwaka huu.
Samata atakuwa akitegemea kupata msaada mkubwa
kutoka kwa nyota mwenzake wa TP Mazembe, Thomas Ulimwengu aliyekuwa
chachu ya ushindi wa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa baada ya kuingia
akitokea benchi.
Safu ya kiungo ya Stars itakuwa ikiongozwa na
Mrisho Ngassa, pamoja na Abubakari Salum ‘Sure Boy’ na Frank Domayo
watakaokuwa na jukumu la kuharibu mipango ya Wamorocco.
Ngome ya Taifa Stars chini ya nahodha kipa Juma
Kaseja, pamoja na mabeki wake, Aggrey Morris na Kelvin Yondani
wanatakiwa kuwa makini na mshambuliaji hatari wa Morocco, Houssine
Kharja aliyeifungia nchi yake mabao mawili hadi sasa.
Kocha Kim Poulsen: “Wachezaji wote wana ari na wapo tayari kisaikolojia. Sina majeruhi ni jambo la kujivunia.”
Tanzania kwa sasa inakamata nafasi ya pili Kundi C
wakiwa na pointi sita na Ivory Coast wakiongoza kwa pointi saba, wakati
Morocco wakiwa nafasi tatu pointi mbili na Gambia ya mwisho na pointi
moja.
Stars ilipata pointi hizo baada ya kuichapa
Morocco 3-1 na Gambia 2-1 nyumbani na kufungwa na Ivory Coast 2-0
ugenini, na kama watashinda leo watajiweka katika nafasi nzuri kabla ya
kuwakaribisha vinara wa kundi nyumbani Juni 16.
Tanzania, haijawahi kufuzu kwa Kombe la Dunia na
fainali zake kubwa kufuzu ni Kombe la Mataifa ya Afrika 1980
walipotolewa hatua ya makundi pamoja na Kombe la Mataifa ya Afrika kwa
wachezaji wa Ndani (CHAN 2009).
Kikosi: Kaseja, Erasto, Kapombe, Yondani, Morris, Abubakar, Domayo, Samatta, Kazimoto, Ngassa, Kiemba.