Badala yake, uamuzi huo ameuacha kwa Serikali
ambayo wiki iliyopita ilihoji hatua ya Cecafa kupeleka mashindano hayo
Sudan, ambako hali ya usalama haijatengemaa hasa katika Jimbo la Darfur.
Wakati anaongea na waandishi wa habari jana, Tenga
alisema kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ina
umuhimu mkubwa na wanaichukulia kwa tahadhari kubwa.
“Siyo Cecafa wala TFF linapofika suala la usalama
hatuwezi tukabishana na Serikali. Tunasubiri jibu la Serikali, kama
wakisema timu ziende basi tutafanya hivyo.” alisema Tenga huku akikwepa
kutoa msimamo wa moja kwa moja kama Mwenyekiti wa Cecafa alipoulizwa
hatima ya Simba, Yanga na Falcon kwenye michuano hiyo iliyopangwa kuanza
Juni 18-Julai 2.
Aliongeza: “Nina matumaini ruhusa hiyo itatolewa,
lakini hatuwezi kupeleka timu bila ruhusa ya Serikali na inapofika suala
la usalama, nchi yoyote ikiamua kujitoa kwa sababu Serikali yake
imeamua isishiriki kwa ajili ya kuhofia usalama, hatutakuwa na pingamizi
lolote na wala hakutakuwa na adhabu.”
Hali ya kukosekana kwa usalama nchini Sudan,
iliwahi pia kuelezwa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa zaman AU na
mpatanishi maalumu wa Umoja wa Afrika katika mzozo wa Darfur, Salim
Ahmed Salim.
“Kuna vikundi vingi vina silaha na licha ya
kutokuwa na uadui na wachezaji, wanaweza kufanya shambulio na kudhuru
kwa nia tu ya kutuma ujumbe bado wapo na wana silaha. Sidhani kama ni
busara sana kwa timu zetu au mashindano kwenda kufanyika huko,” alisema
Salim.
Kutokana na usalama kuwa mdogo, tayari timu tatu
El Merriekh, El Hilali, Tusker ya Kenya zimeshajiondoa kwenye
mashindano, ingawa Tenga alisema ana taarifa ya Tusker kuwa ndiyo pekee
iliyojiondoa.
Timu ambazo zilipangwa kwenye michuano hiyo ni
Merriekh El Fasher (Sudan) Simba (Tanzania) Al Mann (Somalia), APR
(Rwanda), Hilal Kadougli (Sudan) Ahli Shandi (Sudan) Al Nasr (S.Sudan)
Tusker (Kenya) Super Falcon (Zanzibar) Yanga (Tanzania) Express FC
(Uganda) Vitalo (Burundi) AS Port.