Mashabiki wa Simba wameingiwa na wasiwasi
kutokana na kiwango cha chini kinachoonyeshwa na wachezaji wao wapya
katika mazoezi yao kwenye Uwanja wa Kinesi.
Msimu uliopita uongozi wa Simba uliingia mkenge
katika usajili wake wa nyota wa kigeni na kujikuta kwenye wakati mgumu
kutokana na wachezaji hao kushindwa kuisaidia timu hiyo.
Hivi karibuni klabu hiyo imemsajili beki Samweli
Ssenkooni kutoka Uganda, lakini uwezo mdogo ulioonyeshwa na mchezaji
huyo mazoezini umewatia shaka mashabiki wa timu hiyo na kukumbuka ya
msimu uliopita.
Hata hivyo kocha mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni
amewataka mashabiki hao kutokuwa na wasiwasi kwani bado anamwangalia
Ssenkooni kabla ya kutoa uamuzi wake wa mwisho.
“Nawaomba mashabiki wetu wasiwe na hofu juu ya
mchezaji huyo kwani bado tunamwangalia hivyo acha tumpe muda na baadaye
tutatoa uamuzi,” alisema Kibadeni.
Ssenkooni alitua nchini Jumanne iliyopita likiwa ni pendekezo la Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo, Mosses Basena.