come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

Tenga: Mechi Stars haitatibua mkutano TFF

Rais wa Shirikisho la Soka (TFF), Leodegar Tenga amesema mechi ya timu ya taifa (Taifa Stars) dhidi ya Uganda haitaathiri mkutano mkuu wa dharura wa shirikisho hilo uliopangwa kufanyika Julai 13 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam jana, Tenga alisema kuchezwa kwa mechi hiyo hakuwezi kutibua mkutano huo wa marekebisho katiba ya shirikisho hilo ambao pia umepangwa kufanyika Julai 13 jijini humo.

"Hakuna uhusiano baina ya mkutano mkuu na mechi ya timu yetu ya taifa. Isitoshe tuna ajenda moja tu, ambayo tutamaliza mapema. Wale watakaohitaji kuangalia mechi, wataenda uwanjani," alisema Tenga.

"Uzoefu wetu unaonyesha kwamba mkutano mkuu wa TFF unafanyika kwa siku mbili ukiwa na ajenda 14. Siku ya kwanza tunajadili ajenda 12. Ya pili tunamalizia mbili za uchaguzi mkuu na kufunga.

"Kama tunaweza kujadili ajenda 12 kwa siku moja, kwa nini tushindwe kujadili ajenda moja kwa muda huo na watu wakaendelea na shughili zao zikiwamo za kwenda kuangalia mechi?" alihoji Tenga.

Kauli hiyo ya Tenga imetoka ikiwa ni siku chache baada ya baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu na wadau wa soka nchini kuituhumu kamati ya utendaji ya TFF kwamba ina ajenda ya siri kupanga matukio hayo mawili makubwa yafanyike siku moja.

Tenga, ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), amelazimika kuitisha mkutano huo ili kutekeleza maagizo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuunda kamati za maadili.

Alisema lengo lake ni kuhakikisha katiba ya TFF inafanyiwa marekebisho mapema ili uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo ufanyike Septemba 29 ingawa FIFA walishatoa muda uchaguzi huo ufanyike kufikia Oktoba 31 mwaka huu.