Wadau wa mchezo wa ngumi za ridhaa, wamewasilisha barua ya pingamizi kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupinga uchaguzi wa
Shirikisho la Ngumi za Ridhaa (BFT) uliopangwa kufanyika mkoani Mwanza Julai 7.
Katibu Mkuu wa Chama cha Makocha wa Ngumi za
Ridhaa (TABCA), Akaroly Godfrey alisema kuwa hatua ya kupinga uchaguzi
huo imetokana na ukiukwaji wa Katiba ya Shirikisho la Kimataifa la Ngumi
za Ridhaa (AIBA) na lile la Afrika (ABC) ambalo limeelekeza kuwa vyama
vya nchi vinatakiwa kutoa taarifa ya uchaguzi mkuu siku 90 kabla.
Godfrey alisema kuwa BFT haikufanya hivyo kwa
mujibu wa Katiba hiyo kwani uongozi wao ulifikia kikomo miezi kadhaa
iliyopita. Alisema kuwa kinachofanyika sasa ni kuwaweka wapiga kura
kwenye wakati mgumu kwani BFT ilitakiwa kuitisha mkutano mkuu kwa
kugharimia wanachama na si vinginevyo.
Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga pamoja na
kukiri kuwa Godfrey ni mmoja wa wapiga kura katika uchaguzi huo,
alipinga madai hayo kwa kusema hao ndiyo viongozi wanaoleta fujo katika
michezo.