come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA YAACHANA RASMI NA KIIZA

Wakati hadi jana mshambuliaji wa Yanga na timu ya taifa ya Uganda (The Cranes), Hamis Kiiza akisema kuwa kiasi cha mwisho cha fedha ambacho kitamfanya asaini mkataba mpya wa kuwachezea mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara ni dola za Marekani 45,000 (Sh. milioni 70), uongozi wa klabu hiyo umesema kwamba tatizo kubwa linalochelewesha kusainiwa kwa mkataba mpya na nyota huyo ni kiwango cha mshahara anaotaka alipwe kila mwezi.

Kiiza ambaye bado yuko kwao Uganda, alitua Yanga miaka miwili iliyopita kwa dau la dola za Marekani 30,000 (Sh. milioni 50) ambapo alilipwa kwa awamu mbili.

Akizungumza jana Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Seif Ahmed 'Magari', alisema kuwa mbali na fedha hizo za usajili, Kiiza anataka kulipwa mshahara wa mwezi wa dola za Marekani 3,500 (Sh. milioni 5.6) wakati klabu iko tayari kumlipa dola 1,500 (Sh. milioni 2.4).

Magari alisema kwamba kabla ya kuanza mazungumzo na wachezaji kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, klabu iliandaa fungu maalumu kwa kila mchezaji na kiasi hicho cha fedha ndicho kilichopangwa kulipwa kwa mchezaji huyo huku fedha za usajili zikiwa ni dola za Marekani 35,000 (Sh. milioni 55).

Kiongozi huyo alisema kwamba wao wanachoangalia ni kutowaachia viongozi wajao mzigo wa gharama kubwa za uendeshaji pindi uongozi wa sasa utakapomaliza muda wa kukaa madarakani.
Alisema kwa sasa wao hawana kinyongo na mchezaji huyo kwa sababu wanaamini maamuzi yake yanatokana na malengo na mipango aliyojiwekea.

"Ukijumlisha vitu anavyohitaji ni karibu Sh. milioni 100, ametaka dola za Marekani 45,000 za usajili ambazo ziko juu ya mipango yetu, nyumba (Sh. milioni 8), gari (Sh. milioni 10) na mshahara wa dola za Marekani 3,500 ambao haiwezekani kumlipa kwa timu za ukanda huu... hatutaki yawe kama ya Sunzu (Felix) na Simba," Magari aliongeza.

Kiiza aliliambia gazeti hili jana kwa njia ya simu kuwa bado hajafanya maamuzi mengine kuhusiana na hatma yake na kiasi cha fedha alichowaambia Yanga ndiyo cha mwisho.

Alisema vilevile kuwa bado hajapata timu yoyote ya nje ya Uganda kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio lakini wakala wake anaendelea kulifanyia kazi suala hilo.