BENDI kongwe ya muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma (Pichani) imeingia studio kurekodi nyimbo zake mpya zitakazokuwa katika albam moja.
Msemaji wa bendi hiyo, Rajabu Mhamila ‘Super D’, amesema bendi hiyo imeingia studio kukamilisha kurekodi nyimbo zake mpya ukiwa ni mwanzo wa kurejea upya kwa nguvu zaidi.
Alizitaja nyimbo hizo ni ‘Suluhu’ uliotungwa na Shabani Dede, ‘Lipi Jema’ na ‘Baba Kibebe’ wa Eddo Sanga, ‘Nadhili ya Mapenzi’ wa Juma Katundu, ‘Kwa Muumba hakuna Urithi’ na ‘Machimbo.
Alisema baada ya nyimbo hizo kukamilika, zitawekwa kwenye albamu moja kwa ajili ya kuwapa raha mashabiki wao wawapo majumbani.
Super D alisema bendi hiyo kwa sasa imesimamisha maonesho yake kutokana na funga na watarejea siku ya Iddi Mosi katika ukumbi wa DDC Kariakoo.
Alisema siku ya Idd pili watakua TTC Chang’ombe kabla ya kuhamia Zanzibar siku ya Idd Tatu.
Bendi hiyo kwa sasa inatamba na nyimbo zake mbalimbali; imeweka nia ya kukonga mashabiki wa bendi hiyo kwa kupiga nyimbo mpya na zamani ili kila mtu apate burudani. “Unajua bendi yetu ni kongwe lazima itoe burudani ya aina tofauti,” aliongeza Super D.
Bendi hiyo iliyowahi kupata umarufu mkubwa katika miaka ya nyuma imewahakikishia wapenzi wake kurudi kwenye ubora wake kama zamani kutokana na mikakati mbalimbali.