BAADA ya kufanyiwa fitna ukumbi wa wazi wa Garden Breeze Magomeni Dar es Salaam, bendi ya muziki wa dansi ya Extra Bongo ‘Wazee wa Kizigo’, sasa imeanza kutoa burudani kwenye ukumbi wa Meeda, Sinza, jijini, kila Jumapili.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, mkurugenzi wa bendi hiyo, Kamarade Ally Choki (Pichani na wasanii wake), alisema ameamua kupiga Jumapili Meeda ili kuendelea kuwapa burudani wapenzi na mashabiki wake ambao wamemkosa kwa muda toka alipositisha kupiga Garden Breeze miezi kadhaa sasa.
“Kuanzia Jumapili ya leo, naanza kupiga Meeda, kwani uongozi wa Meeda umekubali kufanya hivyo na hiyo haitaharibu ratiba ya kila Jumamosi, nitakuwa napiga kama kawaida na hii ya Jumapili inakuwa ni kama bonanza, kwani ukija na mwenzako unalipa elfu 5,000 tu,” alisema Choki.
Alisema katika kazi kuna changamoto nyingi na licha ya kufanyiwa fitna katika ukumbi wa wazi, anamshukuru Mungu mashabiki wake wanamfuata kokote aendako na hiyo inazidi kumpa ari ya kubadilika kila kunapokucha.
Katika hatua nyingine, mashabiki wa bendi hiyo, sikukuu ya Idd walijikuta wakishindana kuwatuza waimbaji wa bendi hiyo sambamba na wanenguaji wake.
Mmoja wa shabiki ambaye hakuchoka kumwaga ‘noti’, Husna Rashid, alisema hakujipanga kufanya hivyo ila kutokana na jinsi bendi hiyo ilivyoonesha mambo tofauti, alisukumwa kumwaga fedha hizo.
“Mimi sichoki kuituza Extra Bongo, kwani naipenda sana hii bendi na hasa pale Choki anapoimba wimbo wake wa Kikongo na ule wa ‘Mjini Mipango’, anazidi kunikosha sana, maana bila mipango mjini hukai jamani!” alisema.
