Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Canavaro’, amesema kuumia kwa beki Kelvin Yondani na kutolewa nje kulisababisha kuchanganyikiwa na kucheza ovyo kwa dakika 15.
Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam
FC katika pambano la Ngao ya Jamii lililopigwa mwishoni mwa wiki kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Yanga ilijikuta ikiwapoteza
wachezaji wawili baada ya Yondan na kipa Ali Mustafa kuumia kipindi cha
kwanza cha mchezo.
Yondani aliumia katika dakika ya 12 baada ya
kugongana na Barthez wakiwa katika harakati ya kuokoa mpira na nafasi
yake kuchukulia na Mbuyu Twite, wakati Barthez aliumia dakika ya 25 na
nafasi yake kuchukulia na Deogratius Munishi.
Akizungumza mtandao huu Canavaro alisema:
“Ukweli ni kwamba kila mchezaji alichanganyikiwa baada ya Yondan kuumia na kutoka nje moja kwa moja.
“Ilikuwa bado mapema mechi ndiyo kwanza ilikuwa
imeanza, yaani baada ya tukio lile tulikuwa na wakati mgumu kwani mpira
ulikuwa unachezwa eneo letu takribani dakika 15 baada ya hapo ndipo
tukarejea mchezoni.”
Akizungumzia kuumia kwa Barthez, Canavaro alisema
tukio hilo lilikuwa mtihani mwingine kwao kwani walikuwa hawana imani na
Munishi.
“Nikuambie wazi wachezaji wote tuliingiwa na hofu baada Barthez kuumia, unajua Deogratius hajacheza mechi nyingine Yanga.
“Kumbe na yeye alikuwa na hamu ya kuonyesha uwezo
wake, ukweli alionyesha kiwango kikubwa kiasi kwamba mapigo ya moyo
yakashuka na tukamwamini na kuanza kucheza mpira.”