Makosa ya kiutendaji katika klabu ya Simba huenda yakaigharimu timu hiyo kuwakosa nyota wao wawili waliowasajili kutoka Vital'O ya Burundi, Amissi Tambwe (Pichani akisaini) na Gilbert Kaze, baada ya klabu yao kutokuwa tayari kuwaachia hadi baada ya miezi miwili.
Nyota hao walioisaidia Vital'O kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame mwaka huu, bado wana mikataba isiyozidi miezi miwili na klabu yao, na Simba walitarajia kuwasubiri wamalize mikataba hiyo ili wawasajili bure.
Hata hivyo, jambo hilo haliwezekani kama Simba inahitaji kuwatumia nyota hao tangu mwanzo wa msimu huu kwa vile mwisho wa kuwasilisha hati za uhamisho wa kimataifa (ITC) za wachezaji ni Alhamisi hii.
Kama watawasubiri, watalazimika kuanza kuwatumia baada ya usajili wa dirisha dogo.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana, Tambwe na Kaze, wamezuiwa na timu yao hadi viongozi wa Simba watakapokaa meza moja ya mazungumzo na kufikia mwafaka na klabu hiyo ya Burundi la sivyo itawalazimu nyota hao waendelee kuitumikia klabu hiyo hadi mwisho wa msimu wa ligi ya Burundi.
"Wachezaji hao bado wana mikataba isiyozidi miezi miwili, hivyo Simba tulipaswa kuzungumza nao na kuwapa kiasi kidogo cha fedha na wao kuwaruhusu, lakini hatujafanya hivyo ndiyo maana imekaa vibaya upande wetu," alisema kiongozi mmoja wa Simba.
Alieleza kwamba hiyo yote imekuja baada ya kuwasajili wachezaji hao bila ya kufanya mazungumzo na klabu yao kama sheria zinavyoeleza na kila mwaka tatizo hili limeendelea kujirudia ndani ya Simba kwa kuzungumza na wachezaji kwanza.
Tambwe alisema kwamba anafahamu yeye ni mchezaji wa Simba lakini hatakuja nchini kujiunga na wenzake mpaka viongozi wa klabu hizo mbili watakapokaa na kuzungumza.
Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala, hakuweza kupatikana jana kuelezea hatua ambayo klabu yake imefikia.
Lakini mwishoni mwa wiki alieleza kuwa watahakikisha wanakamilisha taratibu ili iweze kuwatumia kuanzia mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Rhino itakayofanyika Jumamosi mkoani Tabora.
Wakati huo huo, kikosi cha Simba juzi kiliibuka na ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya timu ya Kombaini ya Kiomboi katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Wilaya ya Iramba.
Jana jioni timu hiyo ilitarajiwa kucheza mechi nyingine ya kirafiki dhidi ya Kombaini ya mkoa wa Singida na leo itaelekea Kahama, Shinyanga kuweka kambi ya muda.