come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

SIMBA BADO KIBONDE YASHIKWA SHATI TABORA

Simba jana ilianza kwa lawama na majanga msimu mpya wa ligi kuu ya Bara baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na timu ya Rhino Rangers iliyopanda daraja kwa mara ya kwanza na ambayo Wekundu wa Msimbazi walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuifunga.

Mara baada ya pambano hilo kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi hapa, kocha wa Simba Abdallah Kibadeni alisema matokeo hayo yamesababishwa na Abel Dhaira kufungwa magoli ya kizembe langoni mwa timu hiyo ya Msimbazi.
Saddy Kipanga ndiye aliyeifungia Rhino bao la kusawazisha dakika 25 kabla ya filimbi ya mwisho kwa shuti kali la mpira wa adhabu ndogo kutoka mita 20, ambalo lilimpita ubavuni Dhaira katika lango la Simba.
Adhabu ndogo hiyo ilikuwa imetolewa na muamuzi Amon Paul baada ya Issa Rashid 'Baba Ubaya' kumkwatua mchezaji wa zamani wa Simba Nurdin Bakari nje kidogo ya eneo la hatari.
Bao hilo liliamsha shangwe za watazamaji takribani 20,000 waliohudhuria mechi ya kwanza ya ligi kuu ya Bara mjini Tabora katika miaka 14, tangu Milambo iliposhuka daraja 1999.
Jonas Mkude aliifungia Simba bao la kwanza katika dakika ya 12 kwa kichwa kutokana na mpira wa kona iliyopigwa na 'Baba Ubaya' na kuweka matumaini ya kufanya kile ambacho wachambuzi wa soka walitaraji.
Lakini ndoto hiyo ilianza kuingia dosari dakika nane kabla ya mapumziko, wakati Iman Noel alipoifungia Rhino bao la kwanza kwa mpira wa adhabu ndogo kutoka nje kidogo ya eneo la hatari.
Adhabu hiyo ambayo ilimshinda Dhaira kwa staili ile ile ya goli la pili la wenyeji, ilitolewa baada ya beki Mirani Athumani wa Simba kumrukia mgongoni Victor Hangaya.
Mkude aliifungia Simba bao la pili katika dakika ya 41 baada ya muamuzi Paul kuamuru tuta hilo kutokana na Stanslaus Mwakitosi kumuangusha Amri Kiemba ndani ya 18.
Timu zilikuwa:
RHINO: Abdulkarim Mtumwa, Ally Ahmed, Hussein Abdallah, Julius Masunga, Laban Kambole, Stanslaus Mwakitosi, Daniel Manyenya (abbas Mohammed dk.66), Iman Noel, Victor Hangaya, Nurdin Bakari, Sady Kipanga.
SIMBA: Abel Dharia, Nassoro Masoud, Issa Rashid, Miraji Adam, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhani Chombo (Ramadhani Singano dk.62), Ndemla Said, Amri Kiemba, Betram Mwombeki (William Lucian dk.36), Haruna Chanongo.