KIINGILIO cha chini katika mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii keshokutwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga na washindi wa pili, Azam FC kuashiria uzinduzi wa msimu mpya wa 2013/2014 kinatarajiwa kuwa Sh. 7,000.
Kiingilio hicho ni ongezeko la Sh. 2,000 kutoka kiingilio cha chini katika mchezo wa kufunga dimba la Ligi Kuu msimu uliopita, kati ya Simba na Yanga.
Mara ya mwisho; Beki wa Azam, Joackins Atudo kushoto dhidi ya mshambuliaji wa Yanga SC, Hamisi Kiiza katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu, ambayo Yanga ilishinda 1-0. Mambo yatakuwaje Jumamosi Taifa?
Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa kivutio kwa wapenzi wa mpira wa miguu nchini itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni ambapo mshindi atakabidhiwa Ngao.
Iwapo dakika 90 za mechi hiyo hazitatoa mshindi, timu hizo zitatenganishwa kwa mikwaju ya penalti huku asilimia 10 ya mapato ya mechi hiyo yakienda kwa kituo cha kulelea watoto cha SOS.
Kiingilio cha Sh. 7,000 ni kwa viti vya rangi ya kijani na bluu wakati viti vya rangi ya chungwa itakuwa Sh. 10,000, VIP C Sh. 15,000, VIP B Sh. 20,000 na VIP A Sh. 30,000.