come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

YANGA WAENDELEA KUIPINGA ADHABU YA NGASSA, WADAI MAJIBU KUPATIKANA LEO

UONGOZI wa Klabu ya Yanga unatarajiwa kukutana leo kujadili uamuzi ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kumsimamisha mchezaji wao Mrisho Ngasa sambamba na kulipa sh milioni 45 kwa watani zao Simba.


Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako (Pichani) alisema jijini Dar es Salaam juzi kuwa walishindwa kutoa tamko kutokana na kutopata barua rasmi kutoka TFF, lakini sasa imewafikia.

“Barua tumeipata leo na ndiyo maana tulikuwa kimya, kwani tuliona katika vyombo vya habari na kesho ni Jumapili, tunasubiri hadi Jumatatu siku ya kazi tuweze kukaa na kujadili maamuzi hayo ya TFF,” alisema Mwalusako.

Kamati hiyo chini ya mwenyekiti wake Alex Mgongolwa, wiki iliyopita ilipitia usajili wa Ligi Kuu na kumuidhinisha Ngasa kuchezea Yanga, huku ikimsimamisha mechi sita na kumtaka kurejesha sh milioni 30 pamoja na fidia ya asilimia 50 (mil. 15), kwa klabu ya Simba.

Katika hatua nyingine, Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandts, amesema kufungiwa kwa Ngasa kumeharibu programu zake, ikiwamo katika mechi ya Ngao ya Jamii, juzi, walikoshinda bao 1-0 dhidi ya Azam FC.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo, Brandts alisema licha ya kuibuka na ushindi, hakuridhika na matokeo hayo na kama angekuwapo Ngasa, ana imani wangeshinda zaidi ya bao hilo.

Naye Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alikiri kukosekana kwa umakini kwa safu yake ya ushambuliaji iliyokuwa ikiongozwa na John Boko ‘Adebayor’ na Kipre Tichetche ambao walishindwa kuzitendea haki nafasi kadhaa za kufunga, hususani kipindi cha kwanza.

Wakati huo huo, mechi hiyo imeingiza sh 208,107,000 kutokana na mashabiki 26,084 waliokata tiketi. Kila klabu imepata mgawo wa sh 43,731,183.03.