Yanga jana iliendeleza kasi yake ya ushindi katika mechi za kirafiki za
kujiandaa na msimu mpya wakati ilipoifunga Sport Club Villa ya Uganda
kwa magoli 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mrisho Ngassa, Nadir Haroub 'Cannavaro', Didier Kavumbagu na Haruna
Niyonzima kila mmoja alifunga goli moja wakati mabingwa hao wa Ligi Kuu
ya Tanzania Bara walipopata ushindi kama wa mahasimu wao Simba juzi
dhidi ya Waganda hao.
Ngassa, ambaye amerejea Yanga akitokea Simba katika uhamisho wenye utata
ambao utatolewa maamuzi na TFF kesho, alifunga goli la kuongoza la
wenyeji katika dakika ya 7 kwa shuti la mbali lililomshinda kipa wa
Villa, Elungat Martins.
Hata hivyo, goli hilo lilidumu kwa dakika 11 wakati Siraj Jamal
alipoisawazishia Villa baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Yanga
na mabeki wa klabu hiyo ya Jangwani kushindwa kujipanga.
Wenyeji walirejesha uongozi wao katika dakika ya 27 pale Cannavaro
alipoifungia Yanga goli la pili kwa shuti la mbali baada ya kiungo
Mnyarwanda Niyonzima kumuanzishia 'fri-kiki' kwa pasi fupi.
Mshambuliaji raia wa Burundi, Kavumbagu aliifungia Yanga goli la tatu
katika dakika ya 30 akiusukumia wavuni mpira uliorudi baada ya shuti la
Tegete kugonga 'besela' huku kipa wa Villa akiwa amepoteza maboya na
kutoka katika eneo lake.
Matokeo ya 3-1 yalidumu hadi wakati wa mapumziko ya mechi hiyo ambayo
wachezaji wa Villa walionekana hawaelewani huku kipa wao akishindwa kuwa
mwepesi kutokea na kuzuia mashambulizi ya Yanga.
Dakika tano baada ya kipindi cha pili kuanza, Niyonzima alikaribia
kuifungia Yanga goli la nne lakini shuti lake lilipanguliwa kiufundi na
kipa wa Villa, Martins, na kisha Tegete kupiga nje mpira uliorudi na
kumkuta katika nafasi ya kufunga.
Niyonzima aliifungia Yanga goli la nne katika dakika ya 61 baada ya
kuwazidi kasi mabeki wa Villa na kupiga mpira kushoto mwa kipa na
kutinga wavuni.
Villa walikuwa na nafasi ya kupunguza idadi ya magoli katika dakika ya
67 wakati Ronald Muganga alipomtoka beki wa kati Cannavaro lakini
akachelewa kupiga shuti na kumruhusu kipa wa Yanga, Ally Mustapha
'Barthez' kuuwahi mpira na kuudaka.
Villa ambayo ilitisha miaka ya nyuma ikizinyanyasa timu za Tanzania,
juzi pia ilikumbana na kipigo cha magoli 4-1 kutoka kwa Simba kwenye
uwanja huo huo.
Katika mechi zilizopita Yanga, ilizifunga timu za Mtibwa Sugar (3-1) na 3Pillars ya Nigeria (1-0) kwenye uwanja huo pia.
Yanga: Ally Mustapha 'Barthez', Juma Abdul, David Luhende/ Oscar Joshua
(dk.67), Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani/ Rajab Zahir (dk.55),
Athuman Idd 'Chuji'/ Bakari Masoud (dk.67), Mrisho Ngassa, Salum Telela,
Didier Kavumbagu, Jerry Tegete/ Husein Javu (dk.66) na Haruna
Niyonzima/ Said Bahanunzi (dk.66).
Villa: Elungat Martins/ Luyma Sulait (dk.61), Kaggwa Andrew, Baganza
Henry, Kabanda Mike, Kisalita Ayub, Ssempa Charles, Ndaula Moses,
Semboty Godfrey, Siraj Jamal, Muganga Ronald na Kayoya Emima.