Kocha wa Yanga, Ernest Brandts (Pichani), amesema mchezo wa leo wa
ligi kuu dhidi ya timu ya Mbeya City ya hapa utakuwa mgumu kwa mabingwa
wa soka wa Bara hao kutokana na ubovu wa Uwanja wa Sokoine ambao
utawafanya washindwe kucheza mpira waliojifunza.
Alisema kutokana na ubovu huo, hatohitaji wachezaji wake waonyeshe ufundi na badala yake atataka wacheze kulingana na hali ya uwanja huo ilivyo.
Akizungumza kabla ya mchezo wa leo, Brandts alisema ameruhusu wachezaji wasizingatie kupiga pasi zaidi kwa sababu ubovu wa sehemu ya kuchezea ya Uwanja wa Sokoine utawafanya wasiwe huru kuchezea mpira.
Alisema atahitaji kuwatumia zaidi wachezaji wenye nguvu na wasiokuwa na mambo mengi ili kuwakabili wapinzini wao wa leo ambao wanaonekana kuuzoea uwanja wao.
Aidha, kocha huyo raia wa Uholanzi ambaye aliipa Yanga ubingwa wa 23 katika msimu wake wa kwanza nchini alisema timu yake pia itawakosa wachezaji kadhaa tegemeo kutokana na ruhusa, kadi na maheraha.
“Nina wakati mgumu kwa kweli.... Ukiacha suala la wachezaji ambao wapo majeruhi pia hali ya uwanja inasikitisha sana," alisema.
"Tumefanya mazoezi leo (jana) na kila ambacho mchezaji anataka kufanya anashindwa kwa sababu ni ngumu kukotroo mpira katika uwanja wenye mabonde.
"Itatuwia vigumu sana kucheza mpira wetu.”
Brandts alisema kuwa kwenye mchezo wa leo atawakosa Haruna Niyonzima ambaye hajarejea nchini kutoka Rwanda, Simon Msuva ambaye ana kadi mbili za njano na Salum Telela ambaye ni majeruhi.
Mpaka kufikia kabla ya mazoezi ya jana jioni kwenye uwanja huo, Brandts alisema hakuwa na uhakika kama ataweza kuwatumia Athuman Iddi ‘Chuji’ na Kelvin Yondan ambao bado hawajawa fiti baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.
Alisema kuwa ingawa ameongozana na wachezaji hao kuja mkoani hapa, hawajapona kikamilifu kwani Chuji ameendelea kuwa na maumivu ya ndani kwenye mguu wake alioumia akiwa na timu ya taifa wakati ikijiandaa kuikabili Gambia.
“Uhakika ni mdogo wa kuwatumia wachezaji hawa lakini nitaangalia baada ya mzoezi ya leo jioni (jana). Nitakaa kuongea nao ili nijue kama wataweza kucheza," alisema na kueleza zaidi:
"Lakini nisingependa kumtumia mchezaji ambaye hajapona kwa sababu nitakuwa namuahatarisha kupata majeraha zaidi.”
Katika mchezo wa leo, Brandts anategewa kuwaanzisha kwa pamoja wachezaji Jerry Tegete, Didier Kavumbagu kama washambuliaji wawili wa kati huku akimtumia Saidi Bahanuzi kama mshambuliaji atakayekuwa akitokea pembeni.
Homa ya pambano hilo la leo imeonekana kuwa juu katika jiji la Mbeya na vitongoji vyake huku bendera za wenyeji hao wenye pointi nne kama Yanga zikiwa zimetawala katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu kama vituo vikubwa vya magari na maduka makubwa.