come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

FRANSIS CHEKA AOGOPA KUZIPIGA NJE YA NCHI

Bingwa wa dunia wa WBF, Francis ‘SMG’ Cheka (Pichani)  amesema hataki kutetea ubingwa huo wa dunia nje ya Tanzania.


Cheka amekwenda mbali zaidi na kueleza kuwa anahitaji apewe muda wa kutetea taji hilo hapa nchini kwa kile alichodai itamsaidia kulirudisha tena kwenye himaya yake.

“Nikilitetea hapa nchini ni tofauti na itakavyokuwa nje ya nchi kwani nimepigana mapambano mengi nje na mara nyingi naona mabondia wanaokuwa kwao wanavyobebwa.

“Nikiutetea mkanda huu nje ya Tanzania naamini nitanyang’anywa kwani huko hawataweza kukubali kunipa ubingwa wamwache bondia wao,” alisema Cheka.

Cheka anatarajiwa kutetea ubingwa huo mapema Novemba na bondia ambaye atatajwa hapo baadaye, ambapo hata nchi atakayopigania pambano hilo itatajwa baadaye.

Katika hatua nyingine, Cheka ameishukuru Serikali kwa kutambua mchango wake kwenye sekta ya ngumi za kulipwa na kuamua kumwalika bungeni.

Wakati huohuo; kocha wa  Cheka, Abdallah ‘Comando’ Salehe amesema pamoja na changamoto zilizotokea kwenye pambano la bondia wake na Phil Williams wa Marekani lakini promota wa pambano hilo, Jay Msangi amewafungulia njia.

“Msangi anatakiwa kusaidiwa kwani ndiye promota aliyemfungulia njia bondia wangu hadi kupewa heshima ya kuitwa bungeni,” alisema Salehe. Kocha huyo anayetajwa kuwa kocha bora hivi sasa hapa nchini alibainisha kuwa kitendo cha promota huyo kuonekana hafai hivi sasa si cha kiungwana.

“Kilichotokea kinaweza kutokea popote duniani, hata Cheka aliwahi kusotea fedha zake alipokwenda kupigana Ujerumani mwaka jana na hakuna aliyefuatilia hadi leo hajalipwa.

“Bahati nzuri promota huyo amekubali deni hivyo ni kitendo cha kumsaidia na kuangalia ni namna gani atalipa fedha hizo na si kumwona hafai katika jamii,” alisema kocha huyo.