Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen amesema kukosekana kwa wachezaji wake tisa ndiyo chanzo cha kufungwa na Gambia mabao 2-0 katika mechi ya marudiano ya kuwania tiketi ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2014.
Taifa Stars ilifungwa na Gambia juzi katika mechi hiyo iliyochezwa huko Banjul, ambapo kutokana na kipigo hicho, Stars iliyokuwa kundi C ilikamilisha ratiba ikiwa katika nafasi ya tatu nyuma ya vinara Ivory Coast, Morocco, huku Gambia ikikamata mkia.
Akizungumza mjini Banjul, kocha Kim aliwataja wachezaji wake muhimu aliowakosa kuwa ni John Bocco, Athuman Idd, Abubabar Salum, Aggrey Morris, Kelvin Yondan, Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu.
“Kipigo tulichokipata kimechangiwa na kukosekana kwa wachezaji wangu tisa muhimu, tulikuwa katika wakati mbaya kabisa,” alisema Kim.
Alisema, “TFF inapaswa kuhakikisha wachezaji wanaocheza nje wakiitwa kuichezea Taifa Stars wanakuja nyumbani kucheza, nimeambiwa Gambia waliita wachezaji 11 kutoka nje kwa sababu walitambua umuhimu wa kushinda mechi hii, lakini sisi tulikosa karibu wachezaji wa timu nzima.”
Kocha Kim aliongeza kuwa, “Tumeijenga Taifa Stars tukiwa na malengo ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Afrika kwa hiyo ni muhimu sana wachezaji wetu wanaocheza nje wakiitwa waje kuitumikia Taifa Stars.”
Hata hivyo, kocha Kim licha ya kufadhaishwa na matokeo hayo alisema anajivunia faida ya uzoefu ambayo baadhi ya wachezaji wake hasa vijana wameipata katika mashindano hayo ya kufuzu, ambapo anaamini uzoefu huo utakuwa na faida kwa siku za baadaye.
“Mechi hizi za Kombe la Dunia zimetupa uzoefu kwani tumeweza kucheza na timu kubwa kama Ivory Coast na Morocco na kuonyesha uwezo mkubwa zaidi, hii inaonyesha kuwa timu yetu imeimarika kabisa,” alisema Kim.
Alisema hivi sasa macho yake ameyaelekeza katika fainali za Kombe la Afrika 2015, ambapo anataka kukiandaa vyema kikosi chake kuhakikisha kinafuzu kushiriki fainali hizo.
“Inasikitisha, lakini Watanzania lazima waelewe kuwa malengo yangu kwa timu hii ni malengo ya muda mrefu na timu inaendelea kuimarika siku hadi siku,” alisema Kim.
Kwa upande wake, Geoffrey Kaishozi ambaye ni Mtanzania anayefanya kazi Gambia alisema, “Tumesikitika kuwakosa wachezaji wengi tuliowazoea, labda wangekuwapo wangeleta utofauti katika mechi hii.”