come

come
Tuletee habari za kijamii, michezo na burudani, email kabumbu1935@gmail.com

MAKALA: SAID BAHANUZI APANIA KUREJESHA MAKALI YAKE

HUWEZI kuamini kilichotokea msimu uliopita, sijui tuseme alipatwa na tatizo gani lililopelekea kushindwa kung'ara kwenye ligi kuu ya soka Tanzania bara.


Said Bahanuzi mmoja kati ya washambuliaji waliojipatia umaarufu mkubwa kupitia michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki iliyofanyika hapa nchini, Bahanuzi aliibuka kuwa mfungaji bora katika miichuano hiyo baada ya kutupia kambani magoli 6.

Jina lake lilichomoza kimasihara, Aligeuka mfalme ndani ya Yanga ambapo kila sehemu waendapo habari pekee ni Bahanuzi, Hata kikosi hicho kilipokwenda nchini Rwanda kwa mwaliko wa rais wa nchi hiyo Bahanuzi alikuwa gumzo kubwa Rwanda.

Lakini sifa zake na umaarufu wake haukuwa mali kitu kwenmye ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara, mechi 26 zilishindwa kumpa heshima straika huyo aliyesajiliwa toka Mtibwa Sugar.

Alipotua Yanga hakuwa na jina kubwa kama ilivyo kwa nyota wengine wanaosajiliwa na klabu hiyo, Yupo tofauti sana na Hussein Javu ambaye anafahamika kwa shughuri yake ya kucheka na nyavu.

Hata Yanga ilipowaomba Mtibwa kuwa wanamuhitaji Bahanuzi (Pichani), Mtibwa nao waliona ni bora kuwatwisha mzigo Yanga kwani Bahanuzi hakuwa na msaada wowote ndani ya mashamba ya miwa Turiani.

Lakini michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki iliweza kumng'arisha, Aliibuka kinara wa mabao akifuatiwa na Hamis Kiiza pia wa Yanga, ushirikiano wao uwanjani uliinogesha safu ya ushambuliaji ya Yanga iliyokuwa chini ya kocha Mbelgiji Tom Saintfiet.

Yanga ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ikiwa ni kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo tena msimu uliotangulia, Lakini ilipoanza ligi kuu ya bara, Bahanuzi alishindwa kuisaidia Yanga na kujikuta anashindwa kufunga.

Wengi walishangazwa na aina ya uchezaji wake ambapo anapokaribia lango hupiga shuti dhaifu au kupaisha juu, Anafisika kwa mashuti makali lakini yote hayakulenga goli.

Aliwasononesha mashabiki wake ambao tayari wal;ishaanza kumkubali, Mpaka ligi inamalizikka huku klabu yake ikifanikiwa kutwaa ubingwa, Bahanuzi alifunga goli moja tu tena la penalti, Bahanuzi alifunga goli hilo wakati Yanga ilipocheza na Simba kwenye uwanja wa Taifa.

Goli hilo likawa na mwisho kwake na hakuweza kufunga tena hadi ligi inamalizika, Iliwashangaza wadau wengi wa soka na kila moja kuzungumza lake, Msimu mpya wa ligi umeanza rasmi Agosti 24 mwaka huu.

Yanga tayari imeshuka dimbani mara mbili huku ikiwa na mabao 6 ya kufunga, Katika magoli hayo Bahanuzi hakufanikiwa kufunga hata moja, kombinesheni ya Yanga katika safu ya ushambuliaji kwa sasa inawategemea zaidi Didier Kavumbagu na Jerry Tegete.

Ina maana Bahanuzi anaanzia benchi, Lakini katika mechi za majaribio ambazo Yanga ilipata kucheza, Bahanuzi alionyesha kuwa amerejea kwa kasi mpya na kuweza kuwainua wapenzi wa Yanga vitini.

Kwa sasa anauwezo wa kukaa na mpira na kupiga mashuti ya kushutukiza, Ni miongoni mwa washambuliaji wenye nguvu za miguu ambapo mashuti yake huleta presha kwa kipa.

Safu hii haikusita kufanya naye mazungumzo japo kwa ufupi ili kujua hatima yake ndani ya kikosi hicho kinachosaka ubingwa wa 25 wa bara, Bahanuzi alisema kwamba mazoezi ndiyo msingi muhimu wa yeye kurejea kwenye makali yake.

'Kwa sasa najifua sana ili niweze kuwa fiti zaidi, kuhusu kufunga niko makini sana ninapopata nafasi ya kufunga naitumia vema', aliongeza Bahanuzi.

BAHANUZI ATAMBA KUWAKATA VILIMI WANAOCHONGA JUU YAKE

'Dawa yao iko jikoni naamini mwalimu (Ernie Brandts) ndiye anayejua mimi nianze katika kikosi cha kwanza au nianzie benchi, yeye ndiye mwenye kuelewa mchezaji gani yuko fiti, lakini nakwambia wanaochonga juu yangu nitawakata vilimilimi vyao', aliendelea.

Anadai kuwa anapopata nafasi ya kucheza hataki masihara, anatumia nguvu na akili kuweza kulifia lango la wapinzani wake, 'Siku zote ukiwa mshambuliaji unapaswa kutumia nguvu na akili maana mabeki wengi hupendelea kutumia nguvu katika kumnyang'anya mpira adui', alisema Bahanuzi.

BAHANUZI ATOBOA SIRI YA KUWA MFUNGAJI BORA

'Nilishinda kiatu cha dhahabu kutokana na juhudi zangu binafsi pamoja na ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzangu, nina imani kama ushirikiano huo nitaendelea kuupata msimu huu bila shaka nitaibuka mfungaji bora wa ligi kuu ya Tanzania bara', alisisitiza Bahanuzi.

Kuhusiana na timu ya taifa, Bahanuzi amedai hiyo ndio dhamila yake, 'Mchezaji mzuri lazima awepo timu ya taifa, huwezi kuwa mchezaji bora harafu timu ya taifa haupo, Nahakikisha Kim Poulsen ananiita kwenye timu ya taifa kwani ina mapungufu makubwa sehemu ya ushambuliaji', alisema na kuongeza.

'Kila kukicha Watanzania kilio chao ni timu ya taifa, imekosa mshambuliaji mahiri mwenye uwezo wa kucheka na nyavu, lakini mimi nitakuwa suluhisho tosha endapo nitarejeshwa tena kwenye kikosi hicho, unajua msimu uliopita niliandamwa sana na majeraha na ikachangia kukosa mechi muhimu', alisema.

'Tofauti na maneno ya watu kwamba nilishuka kiwango, nilikamiwa sana na mabeki wa timu pinzani na tulipocheza mechi yetu ya tatu na Kagera Sugar mjini Bukoba ndipo nilipoumizwa, Nilikaa benchi muda mrefu na niliporejea nikaumizwa tena', alimaliza.

Huyo ndiye Said Bahanuzi, je atafanikiwa kung'ara msimu huu? au ndio mwisho wake umefika! basi ni suala la kusubiri kisha tuone.