Narietha anakuwa mrembo wa pili kutinga hatua ya 15 bora ya shindano la Redd's Miss Tanzania mwaka huu ambalo fainali zake zitafanyika Jumamosi Septemba 21 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mrembo wa kwanza kutinga hatua hiyo ya pili ni Happiness Watimanywa kutoka Dodoma ambaye wiki iliyopita alishinda taji ya Redd's Miss Photogenic.
Jaji mkuu wa shindano hilo, Ibrahim Mzava, aliyeshirikiana na warembo waliowahi kushiriki fainali za Miss Tanzania miaka ya nyuma, Dotto Nusurupia na Tressy Sospeter, alimtangaza Elizabeth Pert kuwa mshindi wa pili, wa tatu ni Svetlana Nyameyo huku mshindi wa nne ni Happiness Watimanywa na Latifa Mohamed alikuwa wa tano.
Wasanii wa muziki wa kizazi kipya wa kundi la Jambo Squad walipamba onyesho hilo.
Taji la Redd's Miss Tanzania Top Model lilikuwa linashikiliwa na Magdalena Munis ambaye alikuwapo ukumbi na kumvisha taji la maua Narietha.
Akizungumza jana, mratibu wa shindano hilo, Hashim Lundenga, alisema kuwa washiriki wote walionyesha uwezo mkubwa lakini ni lazima mmoja wao aibuke mshindi.
Lundenga alisema kwamba warembo hao walirejea jijini jana mchana na jioni ilikuwa ni siku maalum kwa ndugu na familia zao kuwatembelea kambini.
Aliongeza kuwa leo warembo hao wanatarajia kuendelea na mazoezi mengine kwa ajili ya kujiandaa jukwaani kuwania taji la taifa linaloshikiliwa na Brigitte Alfred.